1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNigeria

Mkutano wa ushirikiano wa Saudi Afrika wafunguliwa Riyadh

9 Novemba 2023

Mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi wa Saudi Arabia na mataifa ya Afrika unaendelea huko mjini Riyadh, masuala mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa nishati wa nchi hiyo na mataifa ya Afrika yameibuliwa.

Saudi Arabien Riad Prinz Khalid bin Salman bin Abdulaziz
Mwana mfalme wa Saudia Arabia Abdulaziz bin Salman ni miongoni mwa watu waliohutubia katika mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Saudia na nchi za Afrika.Picha: Saudi Press Agency/APA/Zuma/picture alliance

Mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Saudi Arabia na mataifa ya Afrika unaendelea huko mjini Riyadh, masuala mbalimbali yameibuliwa ikiwemo ushirikiano wa nishati wa nchi hiyo ya kifalme na mataifa ya Afrika pamoja na mustakabali wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Akihutubia katika mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi wa Saudi Arabia na nchi za Afrika unaofanyika mjini Riyadh, Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia Mohammed Al-Jadaan amesema kwamba mfuko wa maendeleo wa Saudia leo utatia saini mikataba yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 533.

Soma zaidi: Mkutano wa uwekezaji na uchumi kati ya Afrika na Saudia wafunguliwa Riyadh

Katika mkutano huo pia Waziri wa Uwekezaji wa Saudi Arabia Khalid Al-Falih ameeleza kwamba serikali ya kifalme ya Saudia inapanga kuwekeza dola billioni 700 katika sekta ya michezo barani Afrika.

Kwa upande wake, mwanamfalme Abdulaziz bin Salman ambaye ni Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia ametia saini mkataba wa awali wa ushirikiano wa nishati na nchi za Afrika zikiwemo Nigeria, Senegal, Chad na Ethiopia. 

Rais Bola Tinubu kuhudhuria mkutano wa kilele mjini Riyadh

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ni miongoni mwa viongozi wa Afrika wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Saudi-Afrika mjini Riyadh ijumaa hii ili kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa nchi yake yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa ushirikiano wa kiuchumi huko mjini Riyadh kati ya Saudi Arabia na mataifa ya Afrika.Picha: Temilade Adelaja/REUTERS

Msemaji wa ofisi ya rais ameongeza kuwa Nigeria imeanza mpango kabambe wa kuwakaribisha wawekezaji nchini humo.

Nigeria inatafuta uwekezaji zaidi badala ya kutegemea deni la kufufua uchumi wa taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika linalokabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei, uhaba wa fedha za kigeni, sarafu inayoendelea kushuka thamani, ukosefu wa usalama na wizi wa mafuta.

Soma zaidi:Afrika yaitaka Marekani kurefusha mkataba wa AGOA

Rais Tinubu ataongozana hadi Riyadh na ujumbe wa maafisa wa ngazi ya juu serikalini wakiwemo waziri uchumi na fedha, bajeti na mipango ya kiuchumi, Waziri wa mambo ya nje, Waziri wa elimu, na mshauri wa masuala ya usalama wa taifa.

Mbali na hayo, mkutano huo pia umegusia suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani, waziri wa nishati wa taifa hilo la kifalme mwanamfalme Abdulaziz bin Salman amesema kuwa jitihada zaidi zinahitajika kuweza kuwasaidia watu wanaokadiriwa kufikia milioni 800 duniani ambao hawana umeme kabisa. 

Saudi Arabia imesema kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanapaswa kushughulikiwa kwa umakini bila ya kuzididimiza nchi zinazokabiliwa na umaskini wa nishati duniani ingawa maafisa wa Saudi pia wanasema kuwa kuendelea kwa uwekezaji mpya katika hidrokaboni ni muhimu kwa utulivu wa nishati.

Saudi Arabia ambayo ni msafirishaji mkubwa wa mafuta ghafi duniani, ilitangaza mwaka 2021 kuwa inalenga kuacha uzalishaji wa mafuta ifikapo mwaka 2060.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW