Rais Muhammadu Buhari kuongoza majukumu ya wizara ya mafuta
30 Septemba 2015Msemaji wa rais Buhari Garba Shehu, amethibitisha kwamba Buhari atapitisha jina lake kama waziri wa mafuta katika orodha ndefu inayosubiriwa ya Baraza la Mawaziri, itakayowasilishwa bungeni ili ipitishwe baadaye wiki hii.
Hatua hii inafanyika miezi minne baada ya Buhari kuingia madarakani na kuapa kupambana na Ufisadi, katika taifa hilo kubwa la Afrika.
Hapo jana rais Buhari alitoa tangazo hilo mjini New York ambapo amekuwa akihudhuria mkutano wa hadhara kuu wa Umoja wa Mataifa, kuwa atajiteua kama waziri wa mafuta. Naibu Waziri ndiye atakayekuwa anaangalia shughuli za kila siku katika wizara hiyo.
Nigeria ni mzalishaji mkubwa wa mafuta, na kodi itokanayo na bishara hiyo inachangia asilimia 80 ya pesa za serikali. Buhari awali alisema takriban dola bilioni 150 zimeibiwa kutoka wizara hiyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Rais Muhammadu Buhari, aliye na miaka 72, ana nia ya kuiimarisha sekta hiyo ya mafuta kwa kuiweka katika nafasi yake ya juu kama ilivyokuwa awali kabla ya visa vya uwizi na ufisadi kutokea. Nigeria ambayo ni mwanachama wa nchi zinazosafirisha mafuta OPEC imekumbwa na visa vya ufisadi mkubwa katika sekta hiyo ya mafuta tangu mwaka uliyopita vinavyokamua uchumi wa nchi.
Kodi zinazopatikana kutokana na bidhaa hiyo muhimu zinachangia asilimia 90 ya ubadilishanaji wa fedha za kigeni nchini humo.
Rais wa zamani Obasanjo pia aliwahi kuiongoza Wizara ya mafuta
Rais huyo mpya wa Nigeria alikuwa waziri wa mafuta mwaka 1977 akiwa chini ya rais wa zamani Olusegun Obasanjo na akasaidia katika uundwaji wa kampuni ya kitaifa ya mafuta NNPC.
Buhari tayari ameanza kuonesha mabadiliko katika kampuni hiyo kwa kuisimamisha kazi bodi nzima na kutangaza uchunguzi wa ufuatiliaji wa fedha zilizoibiwa pamoja na kumchagua kiongozi mpya atakayeiendesha kwa uwazi.
Hata hivyo ni lazima aweke wazi kwamba kuchanganya majukumu mawili ya urais na uwaziri itakuwa ni mkakati wa muda mfupi wa kufanya mabadiliko.
Kwa upande mwengine rais Obasanjo alikuwa pia waziri wa mafuta wakati alipokuwa rais mwaka 1999 hadi mwaka wa 2007 lakini iwapo Buhari hatofanikiwa kuleta mabadiliko ya kweli katika wizara hiyo basi ni yeye pekee atakayelaumiwa kwa kuwa hakuna waziri wa kumtupia kidole cha lawama.
Mwandishi Amina AbubakarAFP/AP/dpa
Mhariri Josephat Charo