Rais wa Pakistan alivunja bunge na kutoa nafasi ya uchaguzi
10 Agosti 2023Rais wa Pakistan Arif Alvi kwa kushauriana na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif, ameamuru jana jioni kuvunjwa kwa bunge na hivyo kutoa nafasi kwa serikali ya mpito itakayosimamia uchaguzi ambao umemtenga mwanasiasa maarufu nchini humo na Waziri Mkuu wa zamani Imran Khan.
Uamuzi huo umechukuliwa siku tatu kabla ya muhula wa miaka mitano wa Bunge hilo kufikia tamati Agosti 12.
Kwa mujibu wa sheria, baada ya kuvunjwa kwa bunge uchaguzi unatakiwa kufanyika ndani ya siku 90, lakini utawala wa sasa tayari umeonya kuwa huenda uchaguzi huo ukacheleweshwa hadi mwakani.
Wachambuzi wanahofia kuwa kucheleweshwa kwa uchaguzi nchini Pakistan, kunaweza kuchochea hasira ya umma na kuongeza wasiwasi katika taifa hilo lenye silaha za nyuklia na linalokabiliwa pia na matatizo ya kisiasa na kiuchumi.