Rais wa Poland afa katika ajali ya ndege
10 Aprili 2010Rais Lech Kaczynski wa Poland amekufa katika ajali ya ndege iliyotokea leo baada ya ndege yake kuanguka karibu na uwanja wa ndege wa Smolensk, Urusi. Maafisa wamesema kuwa abiria wote 132 waliokuwa ndani ya ndege hiyo wamekufa.
Miongoni mwa waliokufa katika ajali hiyo ni mke wa rais huyo, Maria, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Andrzej Kremer, Mkuu wa majeshi ya Poland, Franciszek Gagor, na Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo, Slawomir Skrzypek. Abiria wengine waliokufa katika ajali hiyo ni wabunge na wanahistoria kadhaa.
Rais huyo wa Poland pamoja na ujumbe wake walikuwa wakielekea katika mji wa Katyn karibu na Smolensk kuhudhuria kumbukumbu ya mauaji ya wafungwa wa vita wa Urusi na Poland waliouawa wakati wa utawala wa kisovieti. Kufuatia kifo hicho, Spika wa bunge la Poland, Bronislaw Komorowski, anachukua madaraka ya nchi hiyo.
Rais Kaczynski aliyezaliwa June 18, mwaka 1949 huko Warsaw alichaguliwa kuiongoza nchi hiyo mwaka 2005 baada ya kupata asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa. Rais huyo alisisitiza umuhimu wa Poland kuimarisha uhusiano mzuri kati yake na Marekani.
Aidha, rais huyo aliuunga mkono mfumo wa kuwa na makombora ya kujilinda uliopendekezwa na rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush. Rais huyo na mkewe ambao wote wamekufa katika ajali hiyo wameacha mtoto mmoja wa kike, Marta.
Mwandishi: Grace Patricia Kabog(AFPE/RTRE/BBC/DPAE)
Mhariri: Othman Miraji