1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Senegal atangaza kulivunja bunge

Angela Mdungu
13 Septemba 2024

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amelivunja bunge la nchi hiyo lenye idadi kubwa ya wabunge wa upinzani. Hatua hiyo inatoa nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi wa mapema wa wabunge.

Bassirou Diomaye Faye amelivunja bunge la nchi hiyo 13.09.2024
Rais wa Senagal Bassirou Diomaye Faye alipolihutubia taifa baada ya kuapishwa Aprili 02, 2024Picha: Sylvain Cherkaoui/AP Photo/picture alliance

Ametoa taarifa hiyo kiwa ni miezi sita baada ya kuingia madarakani. Alitoa tangazo hilo Alhamisi jioni wakati alipohutubia taifa kwa njia ya televisheni na kuwasihi wananchi wakipigie kura cha chake ili aweze kufanya mabadiliko ya kimfumo aliyoyaahidi.

Katika hotuba hiyo Faye alisema, ahadi ya ushirikiano na bunge lenye idadi kubwa ya upinzani imekuwa sawa na ndoto. Ameeleza kwamba sehemu hiyo ya bunge imeamua kuwageuka raia na kuzuia kusudi la kuchaguliwa kwake.

Katika hotuba hiyo Rais Faye alitangaza kuwa, uchaguzi mpya wa bunge umepangwa kufanyika Novemba 17. Wachambuzi wanasema chama cha kiongozi huyo wa Senegal cha PASTEF kina nafasi kubwa ya kupata viti vingi kutokana na umaarufu wake na ushindi alioupata katika uchaguzi wa  rais wa mwezi Machi.

Wapinzani walaimiwa kukwamisha mipango ya serikali ya Faye

Kiongozi huyo mwenye miaka 44, baada ya ushindi wake aliahidi kufanya mabadiliko makubwa katika taifa hilo ili kuboresha hali ya maisha kwa raia, kupambana na rushwa na kufanya mapitio ya vibali vya uvuvi kwa makampuni ya kigeni.

Aliahidi pia kuhakikisha kuwa Senegal inapata sehemu kubwa ya rasilimali za asili kwa ajili ya wananchi wake.

Sambamba na Waziri Mkuu wake Ousmane Sonko, Faye aliongeza matumaini ya vijana wa Senegal ambao robo tatu ya raia wake ni chini ya miaka 35.

Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane SonkoPicha: Sylvain Cherkaoui/AP/dpa

Hata hivyo miezi sita baadaye serikali yake imekuwa ikikwama kutekeleza mipango yake. Rais huyo na Waziri Mkuu wake wamezirusha lawama kwa bunge kuwa ndilo linalokwamisha utakelezaji wa ahadi hizo.

Mwezi Juni, muungano wa vyama vya upinzani bungeni uliufuta mjadala wa bajeti kutokana na mzozo kuhusu ikiwa Waziri Mkuu Sonko anapaswa kuwasilisha mwongozo wa sera zake, huku Sonko akidai kuwa halazimiki kufanya hivyo. Bunge la Senegal lina muda hadi mwishoni mwa mwezi Desemba kupitisha bajeti ya mwaka ujao. lakini uchaguzi mpya bunge huenda ukakwamisha hatua hiyo kufanyika kwa wakati.

Kwa mujibu wa katiba ya Senegal Rais ilimruhusu kulivunja bunge hilo lenye idadi kubwa ya wabunge wa upinzani Septemba 12 na kumpa mamlaka ya kuitisha uchaguzi wa mapema. Hatua hiyo inaweza kumpa wingi wa viti anavyovihitaji ili atekeleze sera zake.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW