1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSierra Leone

Rais wa Sierra Leone asema utulivu umerejea mjini Freetown

27 Novemba 2023

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio amesema hali ya utulivu imerejea nchini humo baada ya kutokea shambulizi dhidi ya kambi ya jeshi kwenye mji mkuu wa taifa hilo mapema jana Jumapili.

Sierra Leone yakumbwa na mapambano ya kijeshi mjini Freetown
Hali imekuwa ya wasiwasi nchini Sierra Leone tangu kutokea shambulio dhidi ya ghala la silaha kwenye mji mkuu, Freetown mnamo Jumapili ya Novemba, 26, 2023.Picha: Umaru Fofana/REUTERS

Akilihutubia taifa kupitia televisheni usiku wa kuamkia leo, rais Bio amesema wote waliopanga na kuongoza shambulizi hilo wamekamatwa na kwamba operesheni za usalama na uchunguzi wa suala hilo vinaendelea.

"Viongozi karibu wote waliokula njama ile wamekamatwa. Operesheni za usalama na uchunguzi zinaendelea," amesema rais Bio katika hotuba yake na akiongeza kuwa serikali yake "itahakikisha wote waliohusika wanawajibishwa".

Mwandishi wa habari wa AFP ameripoti kuwa utulivu ulianza ukirejea polepole katika mji mkuu kufikia Jumapili jioni, lakini vituo vya upekuzi vilivyo na ulinzi mkali wa vikosi vya usalama bado vimesalia.

"Serikali inao udhibiti kamili wa hali ya usalama mjini Freetown, washambuliaji wanajisalimisha," waziri wa habari Chernor Bah aliiambia AFP kabla ya hotuba ya rais Bio.

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimewaonyesha wanaume waliovalia sare za kijeshi wakiwa wamekamatwa na kuwekwa ama kando au ndani ya malori ya kijeshi.

Nini kilitokea na kushuhudiwa mjini Freetown siku ya Jumapili?

Rais Julius Maada Bio wakati wa uchaguzi wa Sierra Leone mnamo mwezi Juni, 2023.Picha: Cooper Inveen/REUTERS

Mapema hapo jana Jumapili serikali ya Sierra Leone ilisema vikosi vyake vya ulinzi vilifanikiwa kulidhibiti kundi la wanajeshi iliyowataja kuwa "wasaliti" waliojaribu kuingia ndani ya ghala la silaha kwenye moja makaazi ya askari mjini Freetown.

Milio ya risasi ilisikika kote kwenye mji huo na serikali ilitangaza mara moja marufuku ya kutembea nje kwa nchi nzima.

Walioshuhudia waliliambia shirika la habari la AFP kuwa walisikia milio ya risasi na milipuko katika wilaya ya Wilberforce ya mji huo mkuu, ambako kuna ghala la kijeshi la kuhifadhi silaha na baadhi ya majengo ya ubalozi.

Mashahidi wengine waliripoti juu ya kurushiana risasi karibu na kambi katika wilaya ya Murray Town, nyumbani kwa jeshi la wanamaji, na nje ya eneo jingine la kijeshi huko Freetown.

Wizara ya habari pia iliripoti mashambulizi mengine dhidi ya magereza mapema siku ambayo yalilazimu vikosi vya usalama kurudi nyuma."Kwa hivyo magereza yalizidiwa" na baadhi ya wafungwa kuachiliwa na wengine "kutekwa nyara", ilisema taarifa ya wizara hiyo.

Video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii ilishiria kwamba idadi kubwa ya wafungwa wametoroka kutoka jela kuu ya nchi hiyo.

Sierra Leone na hali dhaifu ya kiusalama baada ya uchaguzi mkuu

Sierra Leone imo kwenye hamkani tangu kuchaguliwa tena kwa rais Bio wakati wa uchaguzi wa mwezi Juni ambao matokeo yake yalikataliwa na mgombea kinara wa upinzani na hata kutiliwa mashaka na mataifa kadhaa ya kigeni ikiwemo Marekani.

Viunga vya mji mkuu wa Sierra Leone, FreetownPicha: John Wessels/AFP

Maandamano ya kupinga serikali ambayo yalisababisha vifo vya maafisa sita wa polisi na raia wasiopungua 21 Agosti mwaka jana, yalikuwa ni jaribio la kupindua serikali, kwa mujibu wa Rais Maada Bio.

Kumekuwa na mapinduzi 8 ya kijeshi katika kanda ya Afrika Magharibi na Kati tangu mwaka 2020, hali inayodhoofisha demokrasia katika eneo hilo.

Mali, Burkina Faso, Niger na Guinea, ambayo inapakana na Sierra Leone, zote zimeangukia chini ya udhibiti wa kijeshi.

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, imelaani kile ilichokiita jaribio la watu fulani "kuchukua silaha na kuvuruga utaratibu wa kikatiba" nchini Sierra Leone. Nao ubalozi wa Marekani mjini Freetown umesema katika taarifa yake kwamba vitendo kama hivyo haviikubaliki.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW