Rais wa Somalia ataka vikwazo viondolewe
14 Julai 2005Nairobi:
Rais wa serikali ya mpito ya Somalia, Abdullahi Yusuf Ahmed, ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurekebisha vikwazo vya silaha vya miaka 13 ilivyowekewa nchi yake. Amesema kuwa hatua hiyo itarahisisha uwezekano wa kupelekwa jeshi la kulinda amani katika nchi hiyo isiyokuwa na sheria. Baraza la Usalama leo litajadili ombi la nchi za Umoja wa Afrika la vikwazo hivyo kulegezwa ingawaje watu wengi wana wasiwasi kuwa hatua hiyo huenda ikasababisha machafuko zaidi. Rais Yusuf amesema kuwa juhudi za serikali yake za kurudisha uimara katika nchi yake zitakuwa bure iwapo vikwazo hivyo vitaendelea. Ametilia mkazo kwa kusema kuwa hataki vikwazo vyote viondolewe isipokuwa baadhi yake. Umoja wa Afrika mwezi wa Januari mwaka huu umeiamuru Mamlaka ya Maendeleo ya serikali za nchi saba za Mashariki mwa Afrika (IGAD) kupeleka Wanajeshi 10,000 wa kulinda amani Somalia kwa lengo la kuisaidia serikali ya Rais Yusuf iweze kujizatiti nchini humo.