Rais wa Syria atoa msamaha mpya kwa wafungwa
21 Juni 2011Hii ni mara ya pili kwa Rais Assad kutoa msamaha kwa wafungwa katika kipindi kisichopindukia mwezi mmoja. Mwishoni mwa mwezi Mei, aliwasamehe wafungwa wote wa kisiasa waliozuiliwa wakati wa machafuko ya nchini humo. Msamaha wa hii leo, umetolewa siku moja baada ya kiongozi huyo kuahidi kufanya mageuzi kadhaa na kuwa na katiba mpya hivi karibuni.
Katika hotuba yake ya tatu kwa taifa, tangu maandamano ya upinzani kuanza nchini Syria katika mwezi wa Machi, Rais Assad amesema, majadiliano ya kitaifa huenda yakafungua njia ya kufanywa mageuzi katika katiba au kuwa na katiba mpya, lakini akaongezea kuwa hakutokuwepo mageuzi yo yote wakati wa machafuko.
Ahadi zake mpya za mageuzi hazikuweza kuwaridhisha wapinzani wake, walioapa kuendelea na maandamano yao. Mwanasheria maarufu wa haki za binadamu, Anwar al-Bunni alieachiliwa huru mwezi uliopita baada ya kuwa jela miaka mitano amesema, hotuba ya Assad inavunja moyo. Akaeleza kuwa madai muhimu ya umma wala hayakutajwa katika hotuba hiyo na kwamba amepuuza ukweli kuwa nchi hiyo inakabiliwa na mzozo wa kisiasa.
Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Victoria Nuland amesema, kinachohitajiwa hivi sasa ni vitendo na sio maneno: hotuba ni maneno tu. Barani Ulaya, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuimarisha vikwazo dhidi ya Rais Assad kwa sababu ya umwagaji damu unaosababishwa nchini humo katika kupambana na maandamano ya upinzani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle amesema :
"Sisi huku Ulaya tumekubaliana vikwazo zaidi. Kilichobaki ni kupata idhini bayana kutoka Umoja wa Mataifa."
Wakati huo huo,Ufaransa ikizidi kuushinikiza Umoja wa Mataifa, imesema, haiwezekani tena kwa Baraza la Usalama la umoja huo, kuendelea kukaa kimya.
Waziri Mkuu wa Ufaransa, Francois Fillon, alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Paris, akiwa na waziri mkuu mwenzake wa Urusi, Vladimir Puitin alisema, wakati umewadia kwa kila mmoja kuwajibika. Lakini, Urusi mara nyingine tena, imesema, kuwa inapinga kuingilia kati mambo ya ndani ya mataifa huru.
Maandamano ya upinzani yanaendelea nchini Syria tangu Machi 15, licha ya serikali kutumia mabavu dhidi ya wapinzani wake. Kwa mujibu wa makundi ya kimataifa ya haki za binadamu, zaidi ya watu 1,300 wameuawa na zaidi ya 10,000 wengine wamekamatwa kiholela. Rais wa Halmashauri ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Jakob Kellenberger amesema, ombi la kuwa na uhuru wa kutembelea maeneo yaliyokumbwa na maandamano na machafuko katika miezi ya hivi karibuni, limeungwa mkono na serikali ya Rais Assad.
Mwandishi:MartinPrema/dpae,afpe
Mhariri:Abdul-Rahman