1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuAfrika

Rais wa Tanzania aamuru uchunguzi visa vya utekaji, mauaji

9 Septemba 2024

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema ameviamuru vyombo vya usalama nchini humo kufanya uchunguzi wa matukio ya utekaji nyara na mauaji.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. Picha: Presidential Press Service Tanzania

Agizo hilo amelitoa saa chache baada ya mwanasiasa wa chama cha upinzani kupatikana akiwa ameuawa.

Ali Mohamed Kibao, mjumbe wa kamati kuu ya chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA, alitekwa nyara siku ya Ijumaa na watu waliojitambulisha kuwa maafisa wa polisi akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda mji wa mwambao wa Tanga uliopo kaskazini mashariki mwa Tanzania.

Duru zinasema kundi hilo la watu lilisimamisha basi la abiria alimokuwamo Kibao na kumwamuru ateremke na kutokomea naye kusikojulikana. Mwili wake ulipatikana jana Jumapili nje kidogo ya mji wa Dar es Salaam ukiwa na majeraha ya kipigo na tindikali.

Katika ujumbe wa rambirambi alioutoa kupitia mtandao wa kijamii wa X, Rais Samia amesema ameelekeza vyombo vya usalama kuchunguza kisa hicho na vingine vya utekaji nyara na mauaji ambavyo vimeripotiwa nchini humo miezi ya karibuni.