1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Tanzania ahimiza chanjo ya Covid-19 kwa raia

27 Septemba 2021

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewakemea viongozi wa serikali za mitaa kwa kuendeleza migogoro miongoni mwao na hivyo kushindwa kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi likiwemo janga la Covid-19

Ruanda | Samia Suluhu und Paul Kagame
Picha: Rwanda Presidency

Ametoa mfano wa janga la Covid-19 linaloendelea kuwakumba Watanzania, lakini badala ya kulivalia njuga, viongozi wa serikali za mitaa wameendeleza migogoro isio na tija kwa taifa.  Rais Samia ametoa kalipio hilo hii wakati akihutubia  mkutano maalumu wa Jumuiya ya Tawala za mitaa nchini Tanzania, ALAT, uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete Jijini Dodoma.

Amesema kuwa Tanzania imekuwa ikikabiliwa na matitizo mbalimbali ikiwemo tatizo la ugonjwa wa kifua kikuu, UKIMWI na Maralia na kuongeza kuwa magonjwa hayo yameshughulikiwa kwa kiasi kikubwa lakini janga la Covid 19 bado haliangaziwi vya kutosha.

Viongozi wenye dhamana katika serikali za mitaa washughulikie janga la Covid-19

Rais Samia Suluhu Hassan wa TanzaniaPicha: REUTERS

Rais Samia amewaagiza  viongozi waliopewa mamlaka katika serikali za mitaa kwenda kulishughulikia janga hilo, ikiwemo kufanya kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi kwa ajili ya chanjo ili wapate kujikinga na sio kuwalazimisha kuchanja bila kueleweshwa.

Wakati Rais akisisitiza kufanyika kwa kampeni kubwa kwa ajili kuhamasisha chanjo, bado kuna baadhi ya watu wanaendelea kushikilia msimamo wa kutokuchanjwa huku wakielezea mashaka ya usalama wao endapo watapatiwa chanjo hiyo. Madai ya watu hao  yanaelezwa kuwa ni kutokana na serikali kushindwa kutoa elimu ya kutosha kuhusiana na chanjo hiyo ya COVID-19. 

Katika siku za hivi karibuni Tanzania ilibadili msimamo wake wa awali kuwa imedhibiti janga la Corona na kisha kukiri hadharani kuwepo kwa wimbi la tatu la virusi hivyo na kuaanza kufuata maelekezo ya Shirika la Afya duniani WHO ikiwemo kukubali kupokea msaada wa chanjo ya Jonhson and Johnson.

Chanzo: DW Dodoma

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW