1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Samia athibitisha kuibuka kwa ugonjwa wa Marburg

20 Januari 2025

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amethibitisha leo Jumatatu kuzuka kwa ugonjwa wa Marburg baada ya mtu mmoja kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo katika wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.

Tanzania | Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atangaza mripuko wa Marburg nchini TanzaniaPicha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, jijini Dar es Salaam.

Amesema majibu ya sampuli zilizochukuliwa kaskazini mwa nchi hiyo, yameonyesha mtu huyo mmoja ameambukizwa ugonjwa huo unaosababisha kifo kwa asilimia 88, ikiwa mtu hatapata tiba.

Wiki iliyopita WHO iiliripoti kile kilichohisiwa kuwa ni maambukizi ya Marburg, ambao ilisema umewaua watu wanane katika mkoa wa Kagera, lakini maafisa wa afya nchini Tanzania waliipinga ripoti hiyo.

Rais Samia amethibitisha leo kwamba vipimo zaidi vimethibitisha kuwepo kwa kesi ya Marburg na sampuli zingine ishirini na tano zilikuwa hasi.

Kama ilivyo kwa ugonjwa wa Ebola ugonjwa wa Marburg husambaa kwa kugusana kwa karibu na watu wenye ugonjwa huo. Dalili zake ni pamoja na homa, maumivu ya misuli, kuhara na mpaka sasa hakuna chanjo iliyoidhinishwa au matibabu kwa ugonjwa wa Marburg.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW