Rais wa Tunisia aahidi kutaja jina la waziri mkuu mpya
21 Septemba 2021Saed ametangaza mipango ya kuandikwa sheria mpya ya uchaguzi na kuteua uongozi wa muda pamoja lakini pia kuendeleza utawala wa aina yake aliyoupata kupitia hatua ya mwezi Julai iliyoitumbukiza kwenye masuali hali ya demokrasia changa nchini humo.
Katika hotuba yake aliyoitowa Jumatatu usiku, Rais Saied ameahidi kwamba juhudi hizo mpya zitaheshimu haki za Watunisia walizozipigania kwa nguvu pamoja na uhuru na katiba.
Hatua za rais huyo zimekitenga chama kilichotawala muda mrefu nchini humo kinachofuata mrengo wa dini ya Kiislamu, ambacho viongozi wake wanamtuhumu rais huyo kwamba amefanya mapinduzi na kusababisha wasiwasi wa makundi yenye itikadi za Kiislamu kote kwenye ukanda huo.
Wakati Watunisia wamekubaliana na hatua zake, mashirika ya haki za binadamu na wadau wengine wana wasiwasi kuhusu mustakabali wa nchi hiyo ambayo peke yake ndiyo iliyotoka salama kwenye vuguvugu la harakati za kudai mageuzi katika nchi za Kiarabu, kwa kupata mfumo mpya wa kidemokrasia.