Rais wa Ufaransa awahimiza Wairak kulinda uhuru wao
2 Septemba 2020Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwasili mjini Baghdad siku ya Jumatano katika ziara yake ya kwanza rasmi nchini Iraq. Hiyo ni ziara ya kwanza rasmi ya rais Macron katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad na amekutana na Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhim kwa mara ya kwanza tangu alipounda serikali mpya mnamo mwezi Mei.
Rais huyo wa Ufaransa, pia amekutana na Rais wa Iraq Barham Salih. Ziara ya rais Macron inafanyika wakati ambapo taifa hilo linakabiliwa na misukosuko ya kiuchumi pamoja na janga la corona linaloelemeza mzigo mzito katika siasa za nchini Iraq. Kwa upande wake rais wa Iraq Barham Salih amethibitisha mtazamo wa nchi yake kwa kusema Iraq inatamani kuwa na jukumu muhimu katika eneo linalotafuta kuwa na utulivu baada ya kukumbwa na vita na mizozo kwa miaka kadhaa..
Kabla ya kuondoka Beirut, Macron alisema anaelekea Baghdad kuzindua mpango pamoja na Umoja wa Mataifa wa kusaidia mchakato wa Iraq huru. Amesema Wairaq, ambao wameteseka sana, wanastahili haki ya kujiamulia mambo yao kuliko kuwa chini ya mamlaka za kimaeneo au chini ya watu walio na itikadi kali. Aliandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba anakwenda mjini Baghdad na anafurahi kuutembelea mji huo kwa mara ya kwanza kuiunga mkono Iraq wakati ambapo inakabiliwa na changamoto nyingi.
Rais Macron amelihimiza tabaka la kisiasa kuleta mageuzi. Amesema Iraq inakabiliwa na ufisadi, ubadhirifu wa fedha, usimamizi mbaya ambao umevuruga utajiri mkubwa wa mafuta nchini humo na kuwaacha wananchi wakitumukia kwenye umasikini na kukabiliwa na uhaba wa nishati ya umeme na maji.
Mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita Wairak waliandamana kupinga tabaka la wanaisasa ambao wanasema hawawajali. Mamia ya watu waliuawa na maelfu walijeruhiwa katika operesheni kali zilizofanywa na maafisa wa usalama.
Vyanzo:/AP/RTRE