Rais Macron kufanya ziara ya siku nne Afrika ya Kati
23 Februari 2023Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atafanya ziara wiki ijayo, katika mataifa manne ya Afrika ya Kati, wakati Paris ikitafuta njia za kukabiliana na ushawishi unaozidi wa China na Urusi katika kanda hiyo.
Ofisi ya Macron imesema rais huyo atazitembelea Gabon kwa ajili ya mkutano wa kilele wa mazingira, ikifuatiwa na Angola, kisha Jamhuri ya Kongo-Brazaville na mwisho Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Ziara yake inakuja wakati wasiwasi ukizidi mjini Paris juu ya ushiriki unaoongezeka wa Urusi katika mataifa yanayozungumza Kifaransa, sambamba na harakati za China kujijengea ushawishi, ambazo zimedhihirika wazi kwa miaka kadhaa.
Anapanga kuizuru Angola kama sehemu ya harakati za kuimarisha uhusiano wa Ufaransa na mataifa ya Afrika yanayozungumza Kiingereza na Kireno. Macron amesisitiza kwamba Afrika ni ya kipaumbele katika mhula wake wa pili, na Julai mwaka jana alifanya ziara nchini Cameroon, Benin na Guinea-Bissau.