Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy afanya ziara fupi Afghanistan
22 Desemba 2007Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amefanya ziara ya kushangaza mjini Kabul hii leo. Lengo la ziara yake hiyo ni kukutana na rais wa Afghanistan, Hamid Karzai, na baadhi ya wanajeshi wa Ufaransa walio nchini humo katika hatua ya kumdhihirishia kiongozi huyo kwamba Ufaransa inaziunga mkono juhudi za kupambana na ugaidi nchini Afghanistan.
Rais Sarkozy ameanza ziara yake ya muda wa saa tano, kwa kufanya mazungumzo na kamanda wa jeshi la Marekani, jenerali Dan McNeill, anayeongoza kikosi cha jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi, NATO.
Kikosi hicho kinasaidia juhudi za kupambana na wanamgambo wa Taliban na kuleta uthabiti nchini Afghanistan baada ya miongo kadhaa ya vita na itikadi kali ya kidini.
Rais Sarkozy ameandamana na waziri wake wa ulinzi Herve Morin na waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa, Bernard Kouchner. Rais Sarkozy akiwa katika ziara yake ya kwanza nchini Afghanistan tangu alipoingia madarakani mwezi Mei mwaka huu, anatarajiwa kuondoka nchini humo baadaye leo.