Rais Museveni atoa amri ya kusalia majumbani nchini humo
31 Machi 2020Kipindi cha amri ya kutotembea baada ya saa moja hadi saa kumi na moja alfajiri kinaanza kuzingatiwa jioni ya leo Jumanne kwa siku 14 zijazo. Nyakati za mchana watu hawataruhusiwa kuendesha magari yao ila tu yale ya kusafirisha mizigo. Majengo ya maduka hayatafunguliwa isipokuwa tu shughuli za benki, ukusanyaji kodi na uuzaji wa vyakula katika masoko rasmi. Rais Museveni amefafanua kuwa wamechukua hatua hii baada ya kugundua kuwa kuna watu wengi ambao walitoka nje ya nchi na wakakwepa karantini kwa hiyo ni rahisi kwao kuendelea kueneza virusi vya Corona miongoni mwa wananchi.
Akitangaza maagizo hayo siku ya Jumatatu jioni, Museveni aidha ameagiza viwanda kufunga kama haviwezi kuwaweka wafanyakazi katika kambi ya muda eneo la kazini kwao. Katika hatua ya kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara katika kipindi hiki kigumu kiuchumi, kiongozi wa Uganda ameahidi kushauriana na benki, mashirika ya maji na umeme kutowaandama wanaodaiwa kwa sasa wala kuwakatia maji na umeme. Ameahidi aidha kutoa misaada ya chakula kwa familia zinazobainika kuwa husaka riziki zao za kila siku ili kujikimu chakula katika kipindi hiki ambapo Uganda inafanya juhudi kuepusha watu walioingia na virusi hivyo nchini kuwambukiza wengine.
Rais Museveni amewaonya wanasiasa kutojihusisha katika kutoa misaada yoyote ya chakula na mahitaji kwa wananchi kwani wataweza kusababisha mikusanyiko. Atakayepatikana atafunguliwa mashtaka ya jaribio la kufanya mauaji. Tamko hili limefasiliwa kumlenga mpinzani wake Dr. Kizza Besigye ambaye alikuwa ameanzisha mipango ya ugavi wa misaada ya vitu muhimu kwa wananchi.