1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani aomba msamaha kwa ukatili wa Manazi

19 Aprili 2023

Poland imeadhimisha miongo minane tangu kutokea uasi mkubwa zaidi wa Wayahudi dhidi ya uliokuwa utawala wa Manazi nchini Ujerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia

Polen Gedenken 80 Jahre Warschauer Ghettoaufstand | Bundespräsident Steinmeier
Picha: KACPER PEMPEL/REUTERS

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameungana na wenzake wa Poland na Israel, Andrzej Duda na Isaac Herzog, kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 ya uasi wa Ghetto la Warsaw, ambapo amaetumia hotuba yake ya kwanza kwa rais wa Ujerumani kuhutubia tukio hilo, kuomba msamaha kwa uhalifu uliofanywa na taifa lake wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Soma pia: Uasi wa Ghetto la Warsaw, miaka 80 baadae

"Ninasimama mbele yako leo na kuomba msamaha wako kwa uhalifu uliofanywa na Wajerumani hapa," alisema Steinmeier, akizungumza katika sherehe ya kila mwaka iliyofanyika katika wilaya ya zamani ya Wayahudi ya Warsaw.

Rais Duda amesema Wapoland ni mashujaaPicha: KACPER PEMPEL/REUTERS

Rais huyo wa Ujerumani pia amemshambulia mwenzake wa Urusi Vladmir Putin kwa kuanzisha vita nchini Ukraine. Amesema kwa uvamizi wake haramu dhidi ya nchi jirani ya amani na ya kidemokrasia, Rais wa Urusi amevunja sheria ya kimataifa, na kuongeza kuwa vita hivyo vinaleta mateso yasiopimika, vurugu, uharibifu, na vifo kwa watu wa Ukraine.

Sherehe rasmi imefanyika kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashuja wa Ghetto, uliopo eneo yalikotokea mapigano kadhaa ya uasi huo.

Marais Herzog na Duda pia wametoa hotuba, ambapo Rais wa Poland ametoa heshima kwa wale walioshiriki katika uasi huo.

''Kwangu na kwa Wapoland wengi, wapiganaji hao ni ishara ya ushujaa, kujitolea na ujasiri. Ni mashujaa wa Israel, mashujaa wa Wayahudi wote duniani, ni mashujaa wa Poland na Wapoland,'' alisema Rais Duda.

Wayahudi wa Warsaw walianzisha uasi wao wa silaha dhidi ya Manazi Aprili 19, 1943, wakichagua kupigana kuliko kupelekwa katika kambi za kifo. Hicho ndiyo kitendo kikubwa zaidi cha upinzani dhidi ya Wajerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Ujerumani imeomba msamaha kwa uhalifu uliofanywaPicha: Kacper Pempel/REUTERS

"Lazima tukumbuke," amesema rais wa Israel, Isaac Herzog, na kuogeza kuwa kumbukumbu ya mauaji ya Holocaust hayapaswi kulinganishwa. Takribani Wayahudi 7,000 wanakadiriwa kuuawa katika mapambano ma wengine 6,000 katika mioto iliyoanzishwa na Wanazi katika ghetto hilo.

Mwaka mmoja baada ya kuivamia Poland mwaka 1939, Wajerumani waliunda ghetto katika eneo lenye ukubwa wa kilomita tatu za mraba, likiwa ndiyo kubwa zaidi kati ya ma ghetto yote ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Wayahudi wengi walifia ndani kutokana na njaa na magonjwa, huku wengi wa waliosalia wakipelekwa kwenye kambi ya kifo mashariki mwa mji huo mkuu wa Poland.

Soma pia: Poland na miaka 75 ya uasi wa Wayahudi dhidi ya Wanazi

Wakati uasi huo ukitokea, karibu raia 50,000 walikuwa bado wamejificha kwenye maghala ya chini ya ghetto hilo. Wajerumani walizima uasi huo kwa ukatili wa hali ya juu, kwa kuitia moto wilaya nzima na kuigeuza vifusi na majivu.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW