Rais wa Ujerumani Christian Wulff yupo ziarani Uturuki
20 Oktoba 2010Akiwa rais wa kwanza wa Ujerumani kulihutubia bunge la Uturuki ,Christian Wulff aliwasilisha ujumbe uliokuwa wazi kabisa kwa Wajerumani na kwa Waturuki.Hayo anayasema mwandishi wetu Baha Güngor katika maoni yake juu ya ziara ya Rais wa Ujerumani nchini Uturuki.
Ishara hazikuwa nzuri kabla ya Rais wa Ujerumani kuanza ziara yake ya tatu katika chini za nje.
Kwanza nchini Ujerumani mjadala uliojaa mihemko juu ya suala la uhamiaji unaendelea.Pili jarida maaruf la Ujerumani ,"Focus" linalotolewa kila wiki lilichapisha picha katika ukurasa wake wa mbele iliyomwonyesha Rais Wulff akiwa kama Imamu. Alichofanya ,katika hotuba yake ya kuadhimisha mwaka wa 20 tokea Ujerumani iungane tena ni kueleza kwamba kuwapo dini ya kiislamu, nchini Ujerumani ni hali halisi sawa na kuwapo dini za Ukristo na Uyahudi.
Katika hotuba ambayo ni ya kwanza kutolewa na Rais wa Ujerumani kwenye bunge la Uturuki, Christian Wulff alizungumza kauli ya uwazi.
Katika upande mmoja alisisitiza kwa mara nyingine kwamba Uislamu ni sehemu ya Ujerumani. Katika upande mwingine Rais wa Ujerumani aliwataka waturuki watambue ukweli kwamba Ukristo ni sehemu ya Uturuki na kwamba wakristo wa nchi hiyo wapewe uwezekano wote wa kuiadubu dini yao.Hayo ni pamoja na kutoa mafunzo ya makasisi nchini Uturuki jambo ambalo hadi sasa halijawezekana.
Katika hotubya yake Rais wa Ujerumani pia alizungumzia juu ya masuala ya kisiasa; mgogoro wa Cyprus na suala la Armenia.Wulff pia alisisitiza juu ya haki ya Israek kuendelea kuwapo sambamba na haki ya Wapalestina ya kuwa na nchi yao ya itakayotawaliwa katika misingi ya kidemokrasia.
Kwa kusema hayo rais wa Ujerumani alikuwa anatoa ishara ya kumtaka Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aanzishe tena mdahalo na Israel.
Pia inafaa kutilia maanani kwamba rais Wulff hakutoa ahadi tupu kwa Uturuki kuhusiana na nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya. Juu ya suala hilo alitumia busara na kueleza wazi kabisa kuwa,pamoja na kutambua maendeleo ya uchumi na ya demokrasia yaliyofikwa nchini Uturuki,mazungumzo juu ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya lazima yaendelee kufanyika.
Lakini ishara ya wazi kabisa ni ile aliyoitoa kwa wananchi wa Ujerumani wenye nasaba ya kituruki. Amewataka watu hao wajijumuishe na jamii ya Kijerumani.Na mwito aliuotoa juu ya waturuki kujifunza lugha ya kijerumani uliungwa mkono na Rais wa Uturuki Abdullah Gül kabla ya Rais Wulff kuanza ziara ya nchini Uturuki.
Ziara ya siku tano ya Rais wa Ujerumani Christian Wullf nchini Uturuki itasaidia katika kupunguza hali ya kutoelewana baina ya Waturuki na Wajerumani.Njia aliyoitumia ilikubalika vizuri na wenyeji wake na nasaha alizozitoa zilisikika.
Sasa inapasa kusubiri ili kuona iwapo patatokea mabadiliko katika mjadala juu ya suala la uhamiaji nchini Ujerumani unaolekea kwenda mrama.
Mwandishi: Güngör,Baha (DW Tükisch)
Tafsiri: Mtullya Abdu
Mhariri: Josephat Charo