1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ziarani Italia

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
19 Septemba 2019

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameanza ziara yake nchini Italia kwa kupongeza msimamo wa serikali mpya ya mseto ya nchini Italia wa kuunga mkono Umoja wa Ulaya.

Bundespräsident Frank-Walter Steinmeier
Picha: picture alliance/dpa/F. Gambarini

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anafanya ziara ya siku mbili katika miji ya Roma na Napoli nchini Italia. Steinmeier alipokutana na mwenzake wa Italia Sergio Mattarella alisema Umoja wa Ulaya na Ujerumani zinahitaji Italia ambayo kwanza yenyewe ina moyo wa kutangamana pamoja na nchi zingine za Ulaya kwa sababu hatua hiyo itadhihirisha dhamira kubwa ya kusaidia kurekebisha wajihi wa bara la Ulaya, aliongeza kusema anafurahia sana hatua ya Waziri Mkuu Giusseppe Conte na wahusika wote kwenye serikali mpya ya kukubali tena kuendelea na jukumu la kuiongoza Italia.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Horst Seehofer amewashutumu wakosoaji wa shughuli za uokoaji katika bahari ya Mediterania, na amesema serikali mpya ya Italia inaweza kutoa mapendekezo mapya ya mpango wa Umoja wa Ulaya wa kukabiliana na uhamiaji.

Rais wa Italia Sergio MattarellaPicha: picture-alliance/dpa/AP/A. Tarantino

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ambaye yupo mjini Rome amesema Ulaya inahitaji kutafuta njia za kuongeza mshikamano na Italia na kuisaidia kupunguza mzigo wa nchi hiyo uliopo kwa sasa, mwenzake wa Italia Sergio Mattarella amesema amekaribisha utayari wa Ujerumani wa kuwachukua baadhi ya wakimbizi.

Steinmeier, amesisitiza kwamba Italia na Ujerumani zina mahusiano maalum. Kiongozi huyo baadaye atakutana na Waziri Mkuu wa Italia Giusseppe Conte na Paolo Gentiloni Waziri mkuu wa zamani ambaye sasa ndiye kamishna mteule wa Italia kwenye Tume ya Ulaya.

Kabla ya kuwasili nchini Italia, Rais Steinmeier aliliambia gazeti la Italia la "Corriere della Sera” kwamba serikali mpya ya mjini Rome inamaanisha kuwa Italia imerejea kwenye uwanja wa Ulaya. Lengo la ziara ya Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ni kutoa msukumo mpya wa ushirikiano kati ya Ujerumani na Italia kuhusiana na masuala ya Ulaya. Viongozi hao wanatarajiwa kuzungumzia juu ya wahamiaji wanaotumia bahari ya Mediterania na kuhusu Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya.

Chanzo:/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW