1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Ukraine Yanukovich alegeza msimamo

25 Januari 2014

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich, katika kile kinachoonekana kuwa ni hatua ya kuutuliza upinzani, ameahidi kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri pamoja na makubaliano mengine

Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich (kushoto) akishauriana na Afisa wa Umoja wa Ulaya Stefan Füle mjini Kiev
Rais wa Ukraine Viktor Yanukovich (kushoto) na Afisa wa Umoja wa Ulaya Stefan Füle mjini KievPicha: Reuters/Andrei Mosienko/Presidential Press Service

Yanukovich alitoa pendekezo lake wakati akiwahutubia viongozi wa makanisa wakati waandamanaji wakiweka vizuizi zaidi barabarani na kulidhibiti jumba moja la wizara ya serikali katika mji mkuu Kiev.

Upinzani umetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati baada ya mazungumzo na Rais Yanukovich kukosa kupata suluhisho kamili, wakati maandamano ya umma yakisambaa kote nchini humo. Bingwa wa zamani wa ndondi Vitaly Klitschko, kiongozi wa chama cha Udar (Ngumi), amesema mzozo huo unaweza tu kutatuliwa na Umoja wa Ulaya na Shirika la Usalama na Ushirikiano wa Ulaya (OSCE).

“Yanukovich aliamua kutangaza vita dhidi ya watu wake badala ya kusitisha vurumai….lazima akomeshwe“ Alisema Klitschko. Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry alisema katika kongamano la kimataifa la kiuchumi mjini Davos kuwa wajumbe wa Marekani walikutaka na Yanukovich jana nchini Ukraine kumwekea mbinyo wa kumtaka asitishe ghasia, atatue matakwa ya waandamanaji na kuimarisha uhuru wa kidemokrasia. “Tutasimama na watu wa Ukraine”. Alisema Kerry.

Afisa wa Umoja wa Ulaya Stefan Füle (katikati) na viongozi wa upinzani, Vitali Klitschko (kushoto) na Oleh Tyahnybok wakati wa ziara ya KievPicha: picture-alliance/dpa

Mapema Ijumaa, Afisa wa Umoja wa Ulaya Stefan Fule alifanya mazungumzo mjini Kiev na Yanukovich pamoja na mkuu wa utumishi wa umma Andriy Klyuyev. Rais huyo aliahidi kufanya mabadiliko serikalini, kutangaza msamaha kwa waandamanaji waliokamatwa na kuzifanyia marekebisho sheria kali ambazo kupitishwa kwake wiki iliyopita kulisababisha maandamano mapya, ambayo watu watatu wameuawa.

Sheria hizo ambazo zilisainiwa na Yanukovich, zimekosolewa vikali kwa kuwa zinaukandamiza upinzani kwa sababu zinazuia uhuru wa kujieleza na kuweka adhabu kali kwa maandamano yasiyoidhinishwa na serikali. Viongozi wa upinzani wametaka sheria hizo ziondolewe kabisa.

Marekani ilitoa tahadhari ya kutosafiri nchini Ukraine, ikitaja ongezeko la ghasia na kuwaonya raia wa Marekani kukaa kando na maandamano. Maandamano yalisambaa wiki hii hadi kaskazini na magharibi ya Ukraine, na kuashiria mpasuko uliopo kati ya wazungumzaji wa Kirusi na Kiukraine miongoni mwa idadi ya wananchi milioni 45 wa nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni ya Ujerumani jana imemwita balozi wa Ukraine kuhusiana na mgogoro huo. Kwa mujibu wa msemaji wa wizara hiyo, Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinmeier ataelezea wasi wasi unaozidi kuongezeka nchini Ukraine kwa balozi Pavel Klimkin.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW