1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Rais wa Urusi Vladimir Putin yuko ziarani Mongolia

Angela Mdungu
3 Septemba 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin, yuko ziarani Mongolia katika ziara yake ya kwanza kwenye taifa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, tangu ilipotoa waranti wa kukamatwa kwake mwaka uliopita.

Ulaanbaatar | Mongolia
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa Mongolia Ukhnaagiin Khurelsukh wamekutana MongoliaPicha: Sofya Sandurskaya/Sputnik/Kremlin Pool/AP/picture alliance

Baada ya kuwasili Mongolia, Rais Vladimir Putin alipokelewa kwa gwaride la heshima  katika mji mkuu Ulaanbaatar. Amekutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Mongolia Ukhnaagiin Khürelsükh leo Jumanne. Hatua hiyo inajiri bila ya taifa hilo mwenyeji kuonesha dalili yoyote ya kutii miito ya kumkamata Putin.

Kulingana na mashirika ya habari ya Urusi, katika mazungumzo hayo pia, Putin amemualika mwenzake wa Mongolia kuhudhuria mkutano ujao wa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi la BRICS.

Putin ameanza ziara hiyo  inayotafsiriwa kama ukaidi dhidi ya mahakama ya kimataifa ya Uhalifu, Kyiv, mataifa ya magharibi pamoja na makundi ya kutetea haki yaliyotoa wito wa kukamatwa kwake.

Soma zaidi:Ukraine yaitaka Mongolia kumkamata Putin

Anatakiwa na mahakama hiyo kutokana na tuhuma za kuwasafirisha watoto wa Ukraine kinyume cha sheria tangu wanajeshi wake walipoivamia Kyiv mwaka 2022. 

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICCPicha: Florian Görner/DW

Kwa miaka mingi, Urusi imekuwa ikifanya mazungumzo yanayolenga kujenga bomba la gesi lenye uwezo wa kubeba mita za ujazo bilioni 50 kutoka katika mkoa wake wa Yamal kuelekea China kupitia Mongolia. Ukraine ambayo wiki iliyopita iliiitaka Mongolia imkamate Putin wakati wa ziara yake imekasirishwa na ziara hiyo.

Mashambulizi zaidi ya Urusi yaripotiwa ndani ya Ukraine

Kwingineko, mashambulizi ya Urusi huko Zaporizhzhia yamesababisha vifo vya watu watatu,   wawili miongoni mwao ni mama na mtoto wake wa kiume wa miaka minane waliokuwa katika jengo la hoteli.  Mtu wa tatu amefariki katika shambulio la kombora katikati mwa mji wa Dnipro.

Kulingana na maafisa wa Ukraine, mashambulizi hayo yalilenga miundombinu ya reli katika mikoa miwili, pamoja na mtambo wa umeme katika mkoa wa Kaskazini wa Chernihiv. Mamlaka ya reli ya Ukraine imearifu kwamba miundombinu yake iliyolengwa ni katika mkoa wa Kaskazini Mashariki wa Summy pamoja na katikati mwa Dnipropetrovsk.

Katika hatua nyingine jeshi la anga la Ukraine limezidungua droni 27 kati ya 35 za Urusi katika mashambulizi ya usiku wa kuamkia Jumanne.