Rais wa Uturuki awasili Ujerumani kwa ziara ya siku tatu
27 Septemba 2018Ujerumani na Uturuki zinafanya juhudi za kurejesha uhusiano mzuri kati yao, wakati abapo Erdogan anakwaruzana na Rais Trump na wakati ambapo uchumi wa Uturuki unaendelea kudorora kwa haraka. Hapo kesho rais Erdogan atalakiwa rasmi kwa gwaride la kijeshi na mwenyeji wake rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier. Erdogan pia anatarajiwa kukutana na Kansela Angela Merkel.
Uhisiano kati ya Uturuki na washirika wake wa mfungamano wa kujihami wa NATO uliporomoka na kufikia kiwango cha chini kabisa kutokana na hatua ya serikali ya Erdogan ya kuwatia ndani maelfu ya watu katika msako uliofanyika, baaada ya kushindikana kwa jaribio la kuuangusha utawala wa Erdogan mnamo mwaka wa 2016. Baadhi ya watu hao waliokmatwa walikuwa raia wa Ujerumani.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, mara kwa mara amekuwa anasisitiza umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya Uturuki na Ujerumani ambayo ni maskani ya waturuki wapatao milioni tatu. Ujerumani pia inaitegemea Uturuki katika juhudi za kuzuia wimbi la wakimbizi wanaoingia barani Ulaya.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la waandishi habari wasiojali mipaka Christian Mihr wa kanda ya Ujerumani ameitaka serikali ya Ujerumani imbane Erdogan juu ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Uturuki. Pia ameitaka Ujerumani imshinikize rais huyo wa Uturuki ili waandishi habari waliotiwa ndani bila ya makosa waachiwe.
Mkurugenzi huyo amesema serikali ya Ujerumani inapaswa kuitumia fursa hii inayotokana na haja ya Uturuki ya kutaka kurejesha uhusiano mzuri kati ya nchi mbili hizo, kuishinikiza ili uhuru wa vyombo vya habari uweze kuboreshwa nchini Uturuki.
Wakati huo huo maelfu ya watu wanaompinga Erdogan wanadhamiria kufanya maandamano kwenye barabara za jiji la Berlin na nchini Ujerumani kote ili kupinga vitendo vya kukiukwa haki za binadamu nchini Uturuki na pia kupinga hatua za kijeshi zinazochukuliwa na majeshi ya Uturuki dhidi ya wapiganaji wa kikurdi nchini Syria.
Hata hivyo rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema atatumia fursa ya ziara yake nchini Ujerumani kuboresha uhusiano na pia kutoa mwito kwa Ujerumani wa kuimarisha harakati za kupambana na alichokiita makundi ya kigaidi kama vile PKK na jumuiya ya kiongozi wa kidini, Sheikh Fethullah Gulen anaelaumiwa na Erdogan kwa kuhusika na jaribio la kuipindua serikali yake. Ujerumani imeshalikataa ombi la Uturuki juu ya kukiingiza chama cha PKK katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Mwandishi: Zainab Aziz/AP/DPAE
Mhariri: Mohammed Khelef