1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Rais wa Venezuela aamuru jeshi na polisi kushika doria

31 Julai 2024

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameamuru jeshi na polisi kushika doria kote nchini humo kuanzia leo Jumatano.

Vurumai za baada ya uchaguzi nchini Venezuela
Vurumai za baada ya uchaguzi nchini Venezuela. Picha: Jesus Vargas/Getty Images

Hayo yamearifiwa katika wakati shinikizo linaongezeka dhidi yake kufuatia matokeo ya uchaguzi yanayopingwa na upande wa upinzani.

Amri ameitoa usiku wa kuamkia leo baada ya kushuhudiwa siku mbili za maandamano ya umma kupinga ushindi wake katika uchaguzi wa rais uliofanyika siku ya Jumapili. Makabiliano kati ya maelfu ya waandamanaji na polisi yamesababisha vifo vya watu 6 na wengine zaidi ya 700 wamekamatwa.

Mwanasheria Mkuu wa nchi hiyo amesema wale waliokamatwa walifanya vurugu na kuvishambulia vituo vya polisi, ofisi za tume ya uchaguzi na serikali za miji pamoja na hospitali.

Maduro alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Jumapili kwa asilimia 51.2 ya kura lakini upinzani umesema matokeo hayo yamejaa udanganyifu na kwamba mgombea wao ndiye mshindi kwa sababu amepata idadi kubwa ya kura.