1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Burundi afariki dunia kwa COVID 19

Daniel Gakuba
18 Desemba 2020

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya amefariki dunia mjini Paris alipokuwa amewasili kupatiwa matibabu. Kulingana na mtu wa familia yake aliyenukuliwa na shirika la AFP, kifo chake kimetokana na ugonjwa wa COVID-19.

Ehemaliger Präsident von Burundi Pierre Buyoya gestorben
Picha: Thierry Roge/REUTERS

Mtu huyo kutoka familia ya Buyoya ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Burundi aliyekuwa na umri wa miaka 71 aliaga dunia usiku wa kuamkia leo mjini Paris Ufaransa.

Amesema Jumatano wiki iliyopita Buyoya alilazwa katika hospitali moja mjini Bamako-Mali alipokuwa akiishi, ambako alikuwa ameunganishiwa mashine ya kumsaidia kupumua. Hata hivyo, ameendelea kueleza mwanafamilia huyo, alisafirishwa kwa ndege jana kwenda nchini Ufaransa kupata matibabu zaidi, akiwasili mjini Paris hiyo hiyo jana jioni.

Hata hivyo, chanzo hicho cha habari kimeendelea kueleza, alipokuwa akisafirishwa kwa gari la kubeba wagonjwa kuelekea hospitalini, alikata roho akiwa bado njiani. Wanafamilia  kadhaa wengine wa Buyoya wamethibitisha kifo chake bila hata hivyo kuzungumzia maradhi aliyokuwa nayo.

soma zaidi: Burundi: Buyoya apewa kifungo cha maisha kwa mauaji ya Ndadaye

Nchini Burundi, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika Ikulu ya Rais mjini Bujumbura Willy Nyamitwe amesema kupitia ukurasa wake wa twitter, kuwa kifo cha Buyoya kimekwishathibitishwa na hakuna mashaka yoyote tena.

Pierre Buyoya aliiongoza Burundi kwa takriban miaka 13

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya Picha: STR/EPA/picture alliance

Pierre Buyoya aliiongoza Burundi kwa jumla ya miaka 13 katika vipindi viwili tofauti. Kipindi cha kwanza ni kuanzia mwaka 1987 alipoingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi, hadi 1993 alipoachia madaraka baada ya kushindwa katika uchaguzi na mrithi wake Melchior Ndadaye ambaye aliuawa miezi mitatu tu baada ya kushika hatamu za uongozi.

Buyoya alirejea tena mamlakani mwaka 1996 baada ya mapinduzi mengine ya kijeshi, hadi 2003 alipokabidhi tena madaraka baada ya kusaini makubaliano ya amani ya Arusha.

soma zaidi: Burundi yawakamata maafisa wa kijeshi kwa mauaji ya Ndadaye mwaka 1993

Tangu mwaka 2012 Buyoya alikuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika ukanda wa Sahel, wadhifa aliojiuzulu Novemba iliyopita baada ya mahakama nchini mwake kumkuta na hatia ya mauaji dhidi ya mrithi wake Melchior Ndadaye, na kumhukumu kifungo cha ameisha akiwa hayupo nchini. Buyoya alizikanusha shutuma dhidi yake, na kusema kesi hiyo iliendeshwa kisiasa.

Kuuawa kwa Ndadaye, rais wa kwanza wa Burundi kutoka jamii ya Wahutu walio wengi, na wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, kuliitumbukiza Burundi katika mzozo mbaya wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambao uliangamiza maisha ya watu zaidi ya laki tatu.

Chanzo: afpe, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW