Jam. ya Afrika Kati: Rais wa zamani kugombea uchaguzi ujao
26 Julai 2020Chama chake cha Kwa Na Kwa -KNK kimekuwa kinakutana tangu ijumaa iliyopita mjini Bangui na uamuzi huo ulikuwa unatarajiwa. Uamuzi huo unazingatiwa kuwa wa mashaka makubwa katika nchi hiyo iliyoathirika na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kuondolewa madarakani kwa Bozize mnamo mwaka 2013.
Bozize amesema ameukubali uamuzi wa chama chake wa kugombea urais. Ameeleza kuwa chama chake kimeonyesha imani kwake. Ametoa mwito wa umoja katika nchi hiyo iliyogawika vibaya ambapo utawala wa sheria umesambaratika wakati ambapo thuluthi mbili ya nchi inadhibitiwa na makundi ya wanamgambo.
Bozize amewaambia watu wake kwamba yeye atakuwa mjumbe wa kuleta maridhiano ya kitaifa. Amesema anasikitishwa na hali ya huzuni iliyoleta majeraha ya moyoni na pia amesikitishwa kwamba Jamhuri ya Afrika ya Kati haina demokrasia, ukabila umeongezeka na hakuna uongozi wa dola. Rais huyo wa zamani alirejea nchini mwaka uliopita kutoka Uganda.
Rais huyo wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize alitwaa mamlaka nchini mwake mnamo mwaka 2003 baada ya serikali ya hapo awali kupinduliwa. Miaka 10 baadae utawala wake uliangushwa na Michel Djotodia, kiongozi wa kundi la kiislamu la Seleka katika nchi hiyo ambayo wakristo ndiyo wengi.
Tangu wakati huo Jamhuri ya Afrika ya Kati imetumbukia kwenye vurumai ya umwagikaji damu katika msingi wa vita baina ya pande mbalimbali. Katibu mkuu wa chama cha KNK amesema wanamtaka mwanasiasa huyo agombee tena urais kutokana na shida nyingi za wananchi pamoja na mwito wa wanaharakati.
Mnamo mwaka 2013 Ufaransa iliingilia kati kijeshi kuwatimua wanamgambo wa Seleka na kumaliza operesheni hiyo baada ya Faustine ArchangeTouadera kuchaguliwa kuwa rais mnamo mwaka 2016. Rais huyo anaendelea kuongoza kutokana na kusaidiwa na jeshi kubwa la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Zaidi ya askari 13,000 wa Umoja wa Mataifa bado wako katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mnamo mwaka uliopita, Serikali ya nchi hiyo ilitia saini na makundi mbalimbali yanayodai kulinda maslahi ya makundi na dini zao. Hali imetulia kwa jumla licha ya kutokea mapigano ya hapa na pale ya kupigania raslimali za nchi.
Zaidi ya asilimia 25 ya wananchi milioni 4.7 wameyakimbia makaazi yao kutokana na vita. Hata hivyo rais huyo wa zamani bwana Bozize bado amewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa kutokana na kuhusika na mgogoro wa mwaka 2013. Analaumiwa kwa kuwaunga mkono wanamgambo wa kikristo. Bozize mwenyewe amesema hakuna kitakachoweza kumzuia kushiriki katika uchaguzi na kwamba atauomba Umoja wa Mataifa umwondolee vikwazo. Katika kinyanganyiro hicho Bozize atapambana na rais aliyemo madarakani Faustine Archange Touadera.
Wakati huo huo wataalamu wa Umoja wa Mataifa wametanabahisha kwamba uchaguzi huo unaweza kutoa fursa kwa makundi yenye silaha yanayojaribu kuongeza maeneo wanayoyadhibiti. Ripoti ya wataalamu hao imebainisha kuongezeka kwa wapiganaji kutoka nje na hasa Sudan inayopakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Chanzo:/AFP