1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Maldives ahusishwa na mauaji

4 Oktoba 2012

Chama cha rais wa zamani wa Maldives, Mohamed Nasheed, kimewashutumu maafisa wa serikali ya nchi hiyo kwa kujaribu kukihusisha na mauaji ya mbunge wa nchi hiyo, huku machafuko ya kisiasa yakizuka kwenye kisiwa hicho.

Rais wa zamani wa Maldives, Mohamed Nasheed
Rais wa zamani wa Maldives, Mohamed NasheedPicha: picture-alliance/dpa

Wanaharakati wawili kutoka chama cha upinzani cha Maldivian Democratic (MDP) wamekamatwa kutokana na kuhusishwa na mauaji ya mbunge wa nchi hiyo, Afrasheem Ali, aliyekuwa katika chama cha muungano kinachotawala. Taarifa ya chama hicho cha MDP, imeeleza kuwa mashtaka dhidi yao kuhusu mauaji hayo ya kikatili ni ya kutunga.

Msemaji wa polisi, Hassan Haneef, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba wapelelezi walikuwa katika hatua za kufungua mashtaka kuhusu mauaji ya Ali, aliyekuwa anachukuliwa kama mwanazuoni mzuri wa Kiislamu. Haneef amekanusha taarifa kuwa wanaharakati wa MDP wamebambikiwa shutuma hizo.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limelaani vikali mauaji ya mbunge huyo na kuitaka serikali kufanya uchunguzi huru na kuhakikisha kuwa mauaji hayo hayatosababisha ghasia zaidi.

Siku ya Jumanne majaji walitoa amri ya kuitwa mahakamani kwa Bwana Nasheed, ambaye wiki hii alisusia mwanzo wa kesi yake, ambapo anatarajiwa kusomewa mashtaka ya kutumia vibaya madaraka wakati akiwa kiongozi wa nchi hiyo.

Wanne wakamatwa

Wakati hayo yakijiri, polisi nchini Maldives wamesema wamewakamata watu wanne kutokana na mauaji ya mbunge huyo, mauaji ambayo yamesababisha wasiwasi katika kisiwa hicho chenye Waislamu 330,000 wa madhehebu ya Sunni.

Wafuasi wa Rais wa zamani wa Maldives, Mohamed Nasheed, wakiandamana kumuunga mkono.Picha: Reuters

Msemaji wa Polisi, Hassan Haneef amesema kuwa wanaume watatu na mwanamke mmoja wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusu mauaji hayo. Afisa huyo wa polisi amesema huo ni uchunguzi wa awali na kwamba bado hawajatoa utambulisho wa watu hao.

Rais Mohamed Waheed amelaani vikali mauaji ya mbunge huyo, aliyekuwa na umri wa miaka 46. Katika taarifa yake Rais Waheed amesema kuwa serikali yake itatumia kila njia kuhakikisha inawafikisha katika mkondo wa sheria wahusika wa kitendo hicho cha kikatili.

Serikali yatoa wito wa kuwepo kwa umoja

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Maldives, Jameel Ahmed, amewataka wananchi wa kisiwa hicho kuungana pamoja na kusaidia kuzuia vitendo vya kihalifu nchini humo, taifa linalojulikana kama sehemu ya mapumziko kwa wanandoa. Waziri Ahmed amesema licha ya kuwepo tofauti za kisiasa, kila mwananchi anatakiwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Polisi wa doria wakilinda kwenye mji wa Male kuwazuia wafuasi wa Nasheed.Picha: dapd

Mbunge huyo Afrasheem Ali aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na ambaye alikuwa rafiki wa utotoni wa Nasheed, alizikwa kiserikali siku ya Jumanne na nchi hiyo itakuwa katika maombolezo kwa siku tatu.

Nasheed alijiuzulu kukiongoza kisiwa hicho mwezi Februari mwaka huu baada ya kuondolewa madarakani na maandamano ya kuipinga serikali na tangu wakati huo, kisiwa hicho kimekuwa kikikabiliwa na maandamano na ghasia za mara kwa mara.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW