1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mohammed Morsi azikwa baada ya kufariki mahakamani

Daniel Gakuba
18 Juni 2019

Rais wa zamani wa Misri Mohammed Morsi amezikwa leo, baada ya hapo jana kuanguka mahakamani na kuaga dunia. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametaka kufanyika uchunguzi huru, kufahamu sababu halisi ya kifo chake.

Mohammed Mursi ehemaliger ägyptischer Präsident
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Alleruzzo

Wakili wa rais huyo wa zamani amesema Morsi amezikwa leo asubuhi katika makaburi ya Medinat Nasr Mashariki mwa mji mkuu, familia yake ikiwepo. Televisheni ya taifa imesema kifo chake kilisababishwa na mshituko wa moyo.

Morsi, rais wa kwanza wa kiraia wa Misri, ambaye ni wa kwanza pia kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, alianguka katika kizimba chake mahakamani baada ya kujieleza, na aliwahishwa hospitalini ambako ilitangazwa kuwa alikuwa tayari amekata roho.

Tangu alipoangushwa katika mapinduzi ya kijeshi Julai 2013, aliyekuwa waziri wake wa ulinzi Abdel Fattah al-Sisi amechukua hatamu, na amefanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya maelfu ya wanachama na wafuasi wa kundi la Udugu wa Kiislamu, mamia miongoni mwao wakikabiliwa na hukumu ya kifo.

Serikali ya al-Sissi yanyoshewa kidole

Watetezi wa haki za binadamu wanakosoa mazingira ya wafungwa magerezani nchini MisriPicha: picture-alliance/AA

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Misri wamesema yumkini mazingira mabaya gerezani yamesababisha kifo cha Morsi, hali ambayo wanasema ni ukiukaji wa haki za binadamu. Mmoja wao, Amr Magdi wa shirika la Human Rights Watch amesema ''Tunaamini kwamba mazingira mabovu na ya kutengwa aliyowekwa Morsi yanakidhi vigezo vya utesaji kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, na kanuni za msingi za hali ya wafungwa, ambazo serikali ya Misri ilizipuuza kabisa''.

Mwanaharakati huyo ameongeza kuwa anadhani serikali ya al-Sissi imeonyesha dharau ya kupindukia dhidi za haki za msingi za binadamu.

Soma zaidi: Viongozi wa Udugu wa kiislamu wahukumiwa kunyongwa Misri

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu, amesema pia kwa muda mrefu Mohammed Morsi amekuwa akilalamikia ukosefu wa matibabu yanayofaa kwa ugonjwa wa kisukari aliokuwa nao, na kunyimwa ruhusa ya kumuona daktari wake. Awali, mtoto wa Morsi, Abdullah Mohammed Morsi, ameiambia DW kwamba mara ya mwisho familia iliporuhusiwa kumtembelea baba yake ni Septemba mwaka jana.

Erdogan amwita Mohammed Morsi shahidi

Rais wa sasa wa Misri, Abdel Fattah al-SissiPicha: Reuters

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye ni mshirika wa kundi la Udugu wa Kiislamu amemshambulia rais Abdel-Fattah al-Sisi kwa kifo cha Morsi aliyemuita shahidi, na kuzikosoa nchi za magharibi kufumbia macho rekodi yake mbaya kuhusu haki za binadamu.

Naye katibu mkuu wa tawi la kijeshi la Udugu wa Kiislamu Murad Adeileh, akizungumza kutoka nchini Jordan amesema kifo cha Morsi kimetokana na uhalifu, na kitaka ufanyike uchunguzi wa kimataifa. Iran na kundi la kipalestina la Hamas pia wametoa salamu zao za rambirambi.

Mohammed Morsi amekuwa jela kwa miaka 5 iliyopita, na mwaka 2015 alihukumiwa kifo, kwa hatia za ujasusi na kushirkiana na magaidi.

afpe, ape