1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Msumbiji kutoa ushahidi kashfa ya rushwa

17 Februari 2022

Rais wa zamani wa Msumbiji, Armando Guebuza Alhamisi alitarajiwa kutoa ushahidi katika kashfa kubwa ya rushwa nchini humo, kuhusu mikopo ya siri iliyopewa nchi hiyo katika uongozi wake iliyosababisha mzozo wa kiuchumi.

Armando Guebuza
Picha: DW/Romeu da Silva

Nchi hiyo, iliyoorodheshwa miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ilikopa kwa njia isiyo halali dola bilioni 2 sawa na euro bilioni 1.76 mwaka wa 2013 na 2014 kutoka benki za kimataifa ili kununua meli za uvuvi na meli za uchunguzi.

Serikali ilichukua mikopo hiyo bila kulishirikisha bunge la nchi hiyo.

Deni liligundulika 2016

Hata hivyo, deni lililofichwa hatimaye likafichuka mwaka 2016, na kusababisha wafadhili kama Shirika la Fedha la Duniani, IMF kuondoa misaada ya kifedha nchini humo.

Lakini baadaye ukaguzi huru ulifanyika na kubaini dola milioni 500 zimetumika kinyume cha utaratibu na hazijulikani zilipo.

Ndambi Guebuza, mtoto wa rais wa zamani wa Msumbiji, Armando GuebuzaPicha: Romeu da Silva/DW

Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 79, ambaye atakuwa shahidi wa ngazi ya juu zaidi katika kashfa hiyo, alikuwa rais wa Msumbiji kati ya 2005 na 2015.

Mwanawe mkubwa Ndambi Guebuza ni miongoni mwa washtakiwa 19 maarufu wanaokabiliwa na mashtaka hayo. Alikamatwa Februari 2019 na amekuwa kizuizini tangu wakati huo.

Mtoto wa Guebuza akana mashtaka

Mwaka uliopita Ndambi alikana mashtaka ya kupokea rushwa ili kumshawishi baba yake aidhinishe mpango wa kufanikisha mkopo huo wa siri.

Wakati kashfa ya deni la mkopo huo ilipoibuka, Shirika la Fedha Duniani, IMF na wafadhili wengine walisitisha misaada ya kifedha na kusababisha thamani ya sarafu ya nchi hiyo kuporomoka.

Kesi hiyo inaendeshwa katika mahakama maalum iliyoundwa katika gereza lenye ulinzi mkali kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Maputo.

Waziri wa Fedha wa Msumbiji, Adriano Maleiane wiki iliyopita aliiambia mahakama kwamba mtangulizi wake ameficha madeni hayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW