Rais wa zamani wa UEFA Johansson afariki
5 Juni 2019Lennart Johansson , rais wa zamani wa shirikishio la kandanda barani Ulaya UEFA anayeangaliwa kama baba wa mashindano ya Champions League katika bara hilo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89, shirikisho la kandanda nchini Sweden limesema leo Jumatano. "Soka nchini Sweden linaomboleza," shirikisho la soka nchini humo limesema.
Kipindi cha uongozi wa Johansson katika shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA, kuanzia mwaka 1990 hadi 2007, uliingiliana na kuzaliwa kwa Champions League, mashindano makubwa kabisa duniani ya vilabu, na mabadiliko makubwa ya kandanda kuwa biashara kubwa dunia kwa kuwa na mvuto mkubwa na mapato yaliyoelekezwa na mapato kutokana na televisheni.
Tangazo la kifo chake Johansson , akiwa kipenzi cha wengi licha ya sifa yake ya mtu asiyependa mchezo, limekuja muda mfupi tu kabla ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa FIFA mjini Paris ambako wajumbe ikiwa ni pamoja na rais Gianni Infantino walikaa kimya kwa muda wa dakika moja kumkumbuka.
Mtu wa mfano
"Nimevunjika moyo kutokana na taarifa hizi za kuondokewa na Lennart Johansson," Infantino amesema taarifa. alikuwa raifiki na kisima cha hekima kubwa na hamasa. Nitamshukuru milele kwa kuwa nae akiwa rais wa UEFA wakati ninajiunga na shirikisho hilo mwaka 2000.
"Tangu wakati huo , Lennart amekuwa wakati wote mtu wa mfano wa utendaji wa weledi na muhimu zaidi , kwa utu."
Rais wa UEFA Aleksander Ceferin amesema mtangulizi wake alikuwa "mtumishi wa kandanda" ambaye atakumbukwa daima kama "msanifu wa UEFA Champions League". Johansson alionekana mara ya mwisho hadharani katika fainali ya ligi ya Ulaya kati ya Chelsea na Arsenal mjini Baku Mei 29. Alitarajiwa katika fainali ya Champions League kati ya Liverpool na Tottenham Hotspur Juni 1, mjini Madrid lakini hakuweza kuhudhuria.
Alizaliwa Novemba 5, 1929 katika familia ya kawaida mjini Stockholm katika kitongoji cha Bromma, Johansson alipanda ngazi kuanzia akiwa mhudumu kwa mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi. Alianza kuwa kiongozi wa masuala ya mpira wa miguu katika miaka ya 1960, akiwa rais wa klabu kubwa ya Sweden ya AIK, na kisha kuwa mkuu wa shirikisho la kandanda la Sweden kabla ya kuchaguliwa kuwa mkuu wa UEFA mwaka 1990.