1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKorea Kusini

Rais wa zamani wa Korea Kusini Suk Yeol afungwa maisha

19 Februari 2026

Mahakama ya Korea Kusini imemhukumu rais wa zamani Yoon Suk Yeol kifungo cha maisha kwa kuongoza uasi baada ya kutangaza sheria ya kijeshi, hatua iliyotikisa taifa na kuibua mjadala mkali wa kisiasa na kikatiba.

Korea Kusini, Seoul 2024 | Rais Yoon Suk Yeol atangaza sheria ya kijeshi
Mnamo Desemba 3, 2024 Rais Yoon Suk Yeol alihutubia taifa na kutangaza sheria ya kijeshi mjini Seoul, kwa madai ya kulinda utaratibu wa kiliberali dhidi ya Wakomunist. Hivi sasa hatua hiyo imempeleka maisha jela.Picha: South Korean Presidential Office/AFP

Mahakama ya Korea Kusini imemhukumu rais wa zamani, Yoon Suk Yeol, kifungo cha maisha jela kwa kosa la kuongoza uasi kufuatia tangazo lake la kushtukiza la sheria ya kijeshi Desemba 3, 2024, tukio lililosababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kikatiba kuwahi kushuhudiwa nchini humo katika miongo kadhaa.

Waendesha mashtaka walikuwa wameomba adhabu ya kifo — kiwango cha juu zaidi cha adhabu kwa kosa la uasi chini ya sheria za Korea Kusini — wakidai kuwa hatua zake zilikuwa tishio la moja kwa moja kwa misingi ya demokrasia ya taifa hilo.

Katika hukumu yake, Jaji Jee Kui Youn wa Mahakama ya Wilaya ya Kati ya Seoul alithibitisha kuwa shtaka la kuongoza uasi limethibitika, lakini akatupilia mbali madai kwamba Yoon alikuwa ameandaa mpango wa kuanzisha "udikteta wa kudumu.”

Maelfu ya wafuasi wa mwanasiasa huyo wa mrengo wa kihafidhina walikusanyika nje ya mahakama jijini Seoul, wakipiga kelele kudai aachiwe huru na wengine wakipeperusha bendera za Marekani wakitumai kuwa Rais Donald Trump angetumia ushawishi wake kuweka shinikizo la kisiasa.

Wafuasi hao sasa wanatarajia uwezekano wa msamaha wa mapema, jambo ambalo wachambuzi wengi wanasema linaweza kutokea kwa kuzingatia historia ya misamaha ya kisiasa nchini humo.

Rais wa zamani wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol, katika Mahakama ya Wilaya ya Kati ya Seoul kwa ajili ya kusikilizwa kwa hukumu katika kesi yake ya uasi, Februari 19, 2026.Picha: Yonhap/REUTERS

Mwanzo wa mgogoro wa kikatiba

Katika hotuba ya moja kwa moja kwa taifa, Yoon alidai kuwa alitangaza sheria ya kijeshi kulinda mfumo huria dhidi ya upinzani aliouhusisha na wakomunisti na wafuasi wa Korea Kaskazini, ingawa hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.

Wakosoaji wake walimshutumu kwa kutumia sheria ya kijeshi kama silaha ya kisiasa kuokoa urais wake uliokumbwa na kashfa na kuudhibiti upinzani uliokuwa ukikwamisha miswada yake bungeni kwa miezi kadhaa.

Baada ya tangazo hilo, wanajeshi wenye silaha walitumwa kulizingira Bunge la Taifa, wakivunja madirisha na kuingia ndani huku kukiwa na misukosuko midogo kati yao na wabunge waliokuwa wakijaribu kuingia.

Hata hivyo, hali haikugeuka kuwa mapambano makubwa baada ya wabunge kufanikiwa kupiga kura kwa dharura na kufuta amri ya sheria ya kijeshi ndani ya saa chache.

Hatimaye Yoon alisimamishwa kazi, akakamatwa na kufunguliwa mashitaka kadhaa, huku shtaka la uasi likiwa na uzito mkubwa zaidi kisheria.

Hoja ya adhabu ya kifo

Katika hoja zao za mwisho Januari, waendesha mashtaka walisisitiza kuwa Yoon alipanga kwa muda mrefu kuvunja utaratibu wa kikatiba na kusababisha "madhara makubwa na mateso makubwa kwa taifa na jamii.”

Walidai pia kuwa hakuwahi kuomba radhi kwa dhati wala kuonyesha majuto kwa umma.

Maafisa wa polisi wakilinda jengo la mahakama ambako hukumu dhidi ya rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, ilitolewa, Februari 19, 2026, jijini Seoul, Korea Kusini.Picha: Jintak Han/ZUMA/picture alliance

Hata hivyo, wataalamu wengi waliona kuwa adhabu ya kifo isingetekelezwa kwa kuwa Korea Kusini haijatekeleza hukumu hiyo tangu 1997, kutokana na usitishaji usiyo rasmi wa adhabu hiyo.

Mahakama pia iliwahukumu maafisa kadhaa wa kijeshi na polisi waliohusika katika utekelezaji wa amri hiyo, akiwemo waziri wa zamani wa ulinzi Kim Yong Hyun aliyefungwa miaka 30 jela.

Madai ya mvutano na Korea Kaskazini

Waendesha mashtaka walimtuhumu Yoon kwa kuchochea makusudi mvutano na Korea Kaskazini ili kujipatia mtaji wa kisiasa na kuhalalisha mipango yake ya sheria ya kijeshi.

Alidaiwa kuagiza operesheni ya siri ya droni katika anga ya Korea Kaskazini mwaka 2024 kwa lengo la kuibua majibu ya kijeshi kutoka Pyongyang, lakini mkakati huo haukufanikiwa.

Yoon amekanusha mashtaka yote, akisisitiza kuwa hatua yake ilikuwa ndani ya mamlaka ya rais na ililenga kuzuia kile alichokiita "mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na upinzani.”

Katika miezi iliyotangulia tangazo hilo, mzozo kati ya serikali na upinzani kuhusu muswada wa bajeti ulikuwa umefikia kilele, huku Bunge likiwa limekwama kisiasa.

Mbali na kifungo cha maisha, Yoon tayari alikuwa amehukumiwa miaka mitano jela katika kesi tofauti ya kuzuia haki na kuharibu ushahidi.

Wafuasi wa rais wa zamani Yoon Suk Yeol wakiwa nje ya mahakama kushinikiza kiongozi huyo aachiliwe huru, Februari 19, 2026.Picha: Yonhap/picture alliance

Uongozi mpya Korea Kusini

Tangu Juni 2025, Korea Kusini inaongozwa na rais wa mrengo wa kati-kushoto Lee Jae Myung, aliyekuwa kiongozi wa upinzani wakati wa mgogoro huo na mpinzani wa muda mrefu wa Yoon.

Katika tamko kali baada ya hukumu, wakili wa Yoon, Yoon Kab Keun, aliikosoa mahakama akidai hukumu hiyo ilifuata hitimisho lililopangwa na mwendesha mashtaka maalum badala ya kuzingatia kikamilifu ushahidi.

Alisema ana shaka kama wataendelea na rufaa, akidai kuwa utawala wa sheria uko hatarini, kauli iliyoibua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa kisiasa wa taifa hilo.

Hukumu hiyo imehitimisha sura ya giza katika historia ya kisiasa ya Korea Kusini, lakini imefungua ukurasa mpya wa mjadala kuhusu uwajibikaji wa viongozi na nguvu ya katiba katika kulinda demokrasia.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW