1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Zambia asema uchaguzi 'haukuwa hura na wa haki'

14 Agosti 2021

Rais wa Zambia Edgar Lungu ameutangaza kuwa uchaguzi wa Alhamisi wa rais na bunge kutokuwa huru na wa haki kufuatia vurugu katika mikoa mitatu, huku mgombea wa upinzani Hakaindi Hichilema akiongoza matokeo ya awali.

Edgar Lungu Zambia Präsident
Picha: picture-alliance/P.Wojazer

Lungu, ambaye alikuwa anaongozwa na mgombea mkuu wa upinzani Hakainde Hichilema katika matokeo ya awali kutoka tume ya uchaguzi, alisema chama cha Patriotic Front anachokiongoza kilikuwa kinafanya mashauriano kuhusu hatua yake inayofuata.

"Rais Lungu anasema uchaguzi mkuu katika mikoa mitatu, Mkoa wa Kusini, Mkoa wa Kaskazini Magharibi na Mkoa wa Magharibi, ulikumbwa na vurugu, na hivyo kulifanya zoezi lote kuwa batili," ilisema taarifa kutoka ofisini kwake.

Alisema mawakala wa chama cha Patriotic Front katika mkoa wa Kaskazini Magharibi walipigwa na kufukuzwa kutoka vituo vya kupigia kura, "hali ambayo iliziacha kura za chama hicho tawala bila ulinzi" katika mikoa hiyo mitatu.

Mgombea wa upinzani Hakainde Hichilema, maarufu HH, anaongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais.Picha: Salim Dawood/AFP/Getty Images

Akitolea mfano wa kuuawa kwa mwenyekiti wa chama katika mkoa wa Kaskazini Magharibi wakati wa upigaji kura na kifo cha mwanaume mwingine, Lungu alisema vitendo hivyo vya uhalifu vimeufanya uchaguzi mkuu kutokuwa "huru na wa haki".

Lungu aliingiza jeshi kusaidia kuzuwia vurugu wakati vifo hivyo vilipotokea.

Lungu, 64, amekuwa madarakani tangu 2015. Hichilema - maarufu kama  "HH" - ni mfanyabiashara ambaye amekosoa namna rais alivyosimamia uchumi uliomo katika machafuko.

Kelele za mkosaji

Chama kikuu cha upinzani cha UPND kimeyataja malalamiko ya rais Lungu kama hatua ya mwisho ya ukataji tamaa kutoka kwa utawala unaoondoka madarakani.

Chama hicho pia kimewataka wafuasi wake kuyachulia kwa uzito madai ya Lungu, na kuongeza kuwa wakati umefika kulileta taifa pamoja.

Wawekezaji wanafuatilia kwa karibu matokeo ya uchaguzi, ambao ulifanyika siku ya Alhamisi. Taifa hilo la kusini mwa Afrika linakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni na lilikuwa la kwanza barani Afrika kushindwa kulipa madeni yake katika kipindi cha janga la Covid-19 mnamo mwezi Novemba.

Msaada wa shirika la fedha la kimataifa IMF, ambayo tayari umekubaliwa, umesimamishwa hadi baada ya uchaguzi.

Idadi ya wapigakura imeongezeka kwa asilimia 15 zaidi ya mwaka 2016.Picha: Patrick Mainhardt/AFP/Getty Images

Matokeo kutoka majimbo 31 ya uchaguzi kati ya 156 nchini humo, yamempa Hichilema kura 449,699 dhidi ya 266,202 alizopata Lungu, ambaye anawania muhula wa pili wa miaka mitano.

Baadhi ya majimbo yanajumlisha ngome za Lungu, hii ikiashiria kuwa Hichilema amepata nguvu tangu uchaguzi uliyopita mwaka 2016, aliposhindwa kwa tofauti ndogo katika uchaguzi uliokumbwa na madai ya udanganyifu.

Matokeo ya awali yalitarajiwa awali kutolewa Ijumaa. Lakini yalicheleweshwa baada uhesabuji kuendelea hadi usiku kufuatia ushiriki mkubwa na kwa sababu vyama vya siasa vilikataa tarakimu za awali za tume ya uchaguzi katika jimbo moja, ambazo zilitofautiana na zile za wasimamizi waliokuwepo jimboni.

Watu wanaokadiriwa kufikia milioni 7 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa rais na bunge nchini Zambia, taifa la pili kwa uzalishaji wa madini ya shaba barani Afrika.

Askari polisi akijaribu kuzuwi umati wa wapigakura wanaotaka kuingia lango la kituo cha kupigia kura kilichoundwa kwenye shule ya sekondari mjini Lusaka, Agosti 12, 2021.Picha: Marco Longari/AFP/Getty Images

Kuzuwiwa kwa mitandao ya kijamii

Tume ya uchaguzi ya Zambia iliruhusu kituo cha mwisho cha kupigia kura kusalia wazi hadi saa 11 alfajiri siku ya Ijumaa ili kuwapa watu waliopanga foreni kwa saa kadhaa, fursa ya kupiga kura. Uchaguzi huo pia ulishuhudia vurugu katika mikoa mitatu na upunguzaji wa upatikanaji wa huduma za intaneti.


Katika mji mdogo wa Chawama mjini Lusaka, jimbo la ubunge la Lungu, wakaazi walisema wafuasi wa Lungu na Hichilema, wote walidai ushindi na kusherehekea usiku kucha.

Chama cha Lungu cha Patriotic Front kilisema hesabu ya kura ilionesha uitikiaji mkubwa katika ngome zake na kilikuwa na uhakika wa kushinda. Hichilema anagombea kupitia chama cha United National Development.

Kufuatia malalamiko yaliowasilishwa na shirika la haki za binadamu la Chapter One Foundation, mahakama kuu siku ya Ijumaa ilibatilisha uamuzi wa mamlaka ya serikali kuzuwia majukwaa ya mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, Facebook na Instagram.

Picha: MD Mehedi Hasan/Zuma/picture alliance

Linda Kasonde, mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, alisema hakikuwa wazi ni hadi lini uzimaji wa mitandao ya kijamii utaendelea. Baadhi ya watu walisema siku ya Jumamosi kwamba huduma zao za mtandaoni zilikuwa zimerudi.

"Ilienda tena juu. Baadhi ya watu waliripoti kwamba WhatsApp ilishuka lakini walikuwa wanaipata Facebook na Twitter," alisema.

Kwa mujibu wa hukumu ya mahakama ilionekana na shirika la habari la Reuters, Mamlaka ya habari mawasiliano na teknolojia iliamua kuzimwa kwa mitandao Alhamisi, ambayo ndiyo ilikuwa siku ya uchaguzi.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW