1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais William Ruto awaongoza Wakenya, sherehe za Mashujaa

20 Oktoba 2022

Kwa mara ya kwanza tangu kuchukua hatamu za uongozi, Rais wa Kenya William Ruto amelihutubia taifa kwenye sherehe rasmi za mashujaa.

Kenia Nairobi | Feier am Mashujaa Day
Picha: Simon Maina/AFP

Siku hii maalum hutengwa kuwaenzi waliopigania uhuru wa Kenya na kukimaliza kipindi cha ukoloni. Sherehe hizo ziliwaleta pamoja viongozi wa ngazi ya juu serikalini pamoja na kuhudhuriwa na wakili mwanaharakati aliyekuwa uhamishoni Miguna Miguna. 

Uwanja wa bustani ya Uhuru mtaani Langata mjini Nairobi ndiko kulikoandaliwa sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa. 

Wageni walitumbuizwa kwa muziki wa kitamaduni na aina nyengine pia.

Viongozi wa ngazi ya juu serikalini walifika uwanjani mapema akiweko pia wakili na mwanaharakati Miguna Miguna aliyekuwa uhamishoni nchini Canada.

Alikuwa mwingi wa bashasha na kuahidi kuwa amewasili nyumbani kwa wakati. Miguna Miguna alijikuta pabaya baada na serikali iliyopita baada ya kusimamia kiapo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga mwaka 2018 ambapo Odinga alijitangaza kuwa rais wa wananchi.

Rais William Ruto akikagua gwaride la heshima siku ya Mashujaa Oktoba 20, 2022 katika bustani ya Uhuru Gardens jijini Nairobi.Picha: Simon Maina/AFP

Muda mfupi baada ya saa tano asubuhi, Rais William Ruto aliwasili kwenye bustani la Uhuru. Viti vilikuwa vitupu kwani idadi ya waliojitokeza kuhudhuria sherehe za leo ilikuwa ndogo. Hata hivyo Ruto alilikagua gwaride la heshima aliloandaliwa. Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja ndiye aliyewaalika viongozi wa ngazi ya juu jukwaani.

Kwa upande wake, naibu wa rais Rigathi Gachagua alikiri kuwa hali ni ngumu kiuchumi na wakenya wanahangaika. Hata hivyo aliwarai wote kushirikiana kuimarisha hali za wakaazi.

Hii ni mara ya kwanza kwa William Ruto kuhutubia Wakenya katika sherehe ya kitaifa baada ya kuapishwa kuwa rais wa tano wa taifa hilo la Afrika Mashariki. Rais Ruto aliwapongeza wakenya na kuwataja kuwa mashujaa halisi kwa kudumisha amani hata baada ya uchaguzi mkuu.

Sehemu ya graride la heshima lililoandaliwa na jeshi la Kenya kusherehekea Siku ya Mashujaa Oktoba 20, 2022.Picha: Simon Maina/AFP

Ruto ameahidi kuwa wiki ijayo atazindua rasmi makaazi ya bei nafuu mtaani Kibra Soweto B. Makaazi hayo yanadhamiria kuiondoa mitaa ya mabanda iliyoko Kibra.

Ili kuwawezesha wakenya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, Rais Ruto ameahidi kuwa ipo mipango ya kuiongeza sehemu ya kilimo cha kumwagilia maji katika kipindi cha miaka 3 ijayo. Azma ni kupambana na uhaba wa chakula. Lengo la Siku ya mashujaa ni kuwaenzi waliopigania uhuru kulikomboa taifa kutoka kwa minyororo ya ukoloni. Wakenya wana mtazamo upi kuhusu siku hii?

Wapiganaji wa Maumau walikuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa Kenya.

Siku ya mashujaa ilitambulika kama Kenyatta Dei awali kabla ya kubadilishwa mwaka 2010. 

 

Mwandishi: Thelma Mwadzaya, DW Nairobi

Mhariri: Babu Abdalla

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW