1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Kenya aondoa marufuku ya ukataji miti kwenye misitu

3 Julai 2023

Rais William Ruto wa Kenya ameondoa marufuku ya ukataji miti kwenye misitu, amri iliyowekwa mwaka 2018 ili kuisaidia serikali kufikia lengo lake la kuongeza misitu.

Der keniansiche Präsident William Ruto in Südafrika
Picha: Ihsaan Haffejee/AA/picture alliance

Akizungumza katika ziara yake kwenye kaunti ya Nakuru, Rais William Ruto ametangaza kwamba kuondoa marufuku ya ukataji wa miti kwenye misitu ya umma iliyodumu kwa kipindi cha miaka sita ni njia mojawapo ya kuimarisha uchumi wa jamii zinazotegemea misitu.

Wakati huo huo amezidi kuipigia debe sheria ya fedha ya mwaka 2023 ambayo imepata upinzani kutoka kwa wadau mbalimbali. Amri hiyo iliwekwa mwaka 2018, kufuatia mipango ya rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta, ya kuongeza asilimia 10 ya misitu nchini Kenya.

Wanamazingira wanahofia kwamba hatua hii ya Rais Ruto itakwenda kinyume na mpango wake wa upandaji wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Hata hivyo, wafanyabiashara wa mbao wameridhia mpango huo wakieleza kwamba unazinusuru biashara zao ambazo zilikuwa zinaangamia kutokana na kukosa malighafi.

Aidha wataweza tena kutoa nafasi za ajira kwa vijana ambao walipoteza kazi zao wakati biashara ilipoharibika kama alivyosema Francis Maina ambaye ni mmoja wa wafanyibiashara wa mbao.

Soma pia: Maandamano ya mabadiliko ya tabia nchi yafanyika Kenya

Eneo la Masaai katika Kaunti ya Kajiado nchini KenyaPicha: Andrew Wasike/DW

Pamoja na hayo, Rais Ruto na viongozi wanaomuunga mkono wamezidi kuipigia debe sheria ya fedha ya mwaka 2023 licha ya mahakama kuamuru isitishwe kutekelezwa hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani na seneta wa Busia Okiya Omutatah, itakaposikizwa.

Mbunge wa Molo Kuria Kimani  amesema sheria hiyo haijakiuka kiepengele chochote cha katiba. Amesema baadhi ya wabunge hawakuwa na ufahamu wa kile walichokuwa wakikipinga.

Ruto akosoa hatua ya upinzani

Rais Ruto amekosoa vikali hatua ya muungano wa upinzani ya kurejelea maandamano akisema haitoi suluhu kwa matatizo ya wananchi.

Soma pia: Afrika kuanza kutumia satalaiti kwa mazingira, tabianchi

Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, ameshikilia kuwa maandamano yatafanyika siku ya ijumaa wiki hii ambayo ni maadhimisho ya Saba Saba, kulalamikia hatua alizochukua Rais Ruto zinazomkandamiza mwananchi.

(Wakio Mbogho, DW-Nakuru)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW