1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Xi apongeza utawala wa chama cha Kikomunisti

16 Oktoba 2022

Rais wa China, Xi Jinping Jumapili ameufungua mkutano mkuu wa chama tawala cha Kikomunisti na amekipongeza kwa kusimamia utulivu wa kijamii na kulinda usalama wa taifa.

Peking KP Nationalkongress Xi Jinping
Picha: Thomas Peter/REUTERS

Xi ambaye anatarajiwa kushinda muhula wa tatu wa uongozi kwa miaka mingine mitano na kuimarisha nafasi yake kama mtawala mwenye nguvu zaidi nchini humo tangu enzi za Mao Zedong, aliingia kwenye ukumbi wa Great Hall of the People, uliopo katika jengo la serikali kwenye ukingo wa magharibi wa Uwanja wa Tiananmen katikati ya mji mkuu wa China, Beijing, majira ya saa nne kamili asubuhi kwa saa za China na kuanza kuhutubia.

Rais Xi, mwenye umri wa miaka 69, amepongeza utawala wa chama chake cha Kikomunisti na kuelezea mafanikio yake, ikiwemo usalama wa taifa, kudumisha utulivu wa kijamii pamoja na kuwalinda watu. Kiongozi huyo anatarajiwa pia kuainisha vipaumbele vya miaka ijayo.

''Mkutano mkuu wa 20 wa kitaifa wa chama cha Kikomunisti cha China ni muhimu sana na unafanyika katika wakati muhimu ambapo chama chote na watu wa makabila yote wanaanza safari mpya ya kuijenga kikamilifu nchi ya kijamaa ya kisasa na kuelekea kwenye lengo la karne ya pili,'' alifafanua Xi.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa 20 wa chama tawala cha Kikomunisti cha ChinaPicha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mbele ya zaidi ya wajumbe 2,300 wa chama hicho kutoka nchi nzima, wanaohudhuria mkutano huo utakaofanyika kwa wiki nzima, Xi amesema China imefanikiwa kuidhibiti kikamilifu Hong Kong, na kuigeuza kutoka kuwa yenye vurugu hadi kuwa na utawala. Hong Kong ilikumbwa na maandamano ya kuipinga serikali mwaka 2019.

Amesema China pia imeendesha mapambano makubwa dhidi ya hatua ya Taiwan kutaka kujitenga. ''Tumeonesha azma yetu na uwezo wa kulinda mamlaka ya serikali na uadilifu pamoja na kupinga uhuru wa Taiwan,'' alisisitiza Xi.

Rais huyo wa China amesema chama cha Kikomunisti chenye wanachama milioni 96, ''kimepata ushindi mkubwa dhidi ya umaskini katika historia ya mwanadamu.'' 

Umuhimu wa sera ya COVID-19

Xi pia amesisitiza kuhusu sera za China kuhusu ugonjwa wa COVID-19 ambazo bado zimeweka masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona. Amesema sera hizo ikiwemo kutokuwa na kisa hata kimoja cha ugonjwa wa COVID-19, zimelinda usalama na afya za watu katika kiwango kikubwa na kupata matokeo mazuri.

Kuhusu masuala ya uchumi, Xi amesema China itaunga mkono uchumi binafsi na kuruhusu soko kuchukua nafasi muhimu katika ugawaji wa rasilimali. Amebainisha kuwa China italenga kuwa na ukuaji wa uchumi wa hali ya juu na miaka mitano ijayo itakuwa muhimu kwa kujenga nguvu za kisasa za ujamaa.

Rais huyo wa China ameangazia pia mapambano yake dhidi ya ufisadi, huku akisema yamefanikiwa kuondoa hatari kubwa iliyojificha ndani ya chama tawala cha Kikomunisti na jeshi la nchi hiyo. ''Mapambano dhidi ya ufisadi yamepata ushindi mkubwa na yameimarishwa kikamilifu,'' Xi amewaambia wajumbe wa mkutano huo.

Wajumbe waliohudhuria Jumamosi kikao cha maandalizi ya mkutano mkuu wa chama tawala cha Kikomunisti cha ChinaPicha: Huang Jingwen/Xinhua via AP/picture alliance

Xi amegusia pia suala la mazingira na hali ya hewa, akisema China itashiriki kikamilifu katika juhudi za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkutano huo unatarajiwa kumuidhinisha Rais Xi kuwa katibu mkuu wa chama cha Kikomunisti, nafasi yenye nguvu zaidi nchini China pamoja na kuwa mkuu wa Kamisheni Kuu ya Kijeshi.

Mwishoni mwa mkutano huo mkuu, Xi anatarajiwa kulizindua kundi lake jipya la uongozi lenye watu saba, Kamati ya Kuu ya Chama cha Kikomunisti, Politburo. Aidha, atamchagua mrithi wa Li Keqiang kuwa waziri mkuu, ambaye atasimamia serikali ya taifa hilo lenye chama kimoja cha siasa.

Hakuna mabadiliko muhimu ya sera

Kwa mujibu wa wachambuzi Xi, ambaye amekuwepo madarakani tangu 2012, hatarajiwi kufanya mabadiliko yoyote makubwa na muhimu katika mwelekeo wa sera. 

Aidha, uhusiano wa China na mataifa ya Magharibi umezorota sana, na hasa kutokana na hatua ya Xi kumuunga mkono Rais wa Urusi, Vladmir Putin.

Katika uongozi wake uliodumu kwa muongo mmoja, Xi, ameiweka China kwenye njia inayozidi kuonesha utawala wa kimabavu ambao umetanguliza usalama, udhibiti wa hali ya uchumi, diplomasia yenye uthubutu zaidi pamoja na jeshi imara lenye nguvu.

(AFP, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW