Hatimaye Rais Yoon Suk Yeol akubali kujisalimisha Korea
15 Januari 2025Matangazo
Rais wa Korea Kusini aliyeondolewa madarakani na bunge na kushtakiwa, Yoon Suk Yeol amekamatwa leo Jumatano kama sehemu ya uchunguzi wa tuhuma za kufanya uasi.
Rais Yoon ambaye amehojiwa na maafisa wa Korea Kusini kuhusu uhalifu huo amesema ametowa ushirikiano kwa sababu tu ya kile alichokiita uchunguzi haramu ili kuepusha vurugu.
Soma pia: Wachunguzi Korea wasitisha jaribio la kumkamata Rais Yook
Anatarajiwa kuendelea kushikiliwa rumande akiwa kwenye chumba cha mahabusu kilichotengwa. Ni mara ya kwanza nchini Korea Kusini kwa rais aliyeko madarakani kukamatwa na hatua hii ni mpya kwa taifa hilo lenye demokrasia inayokuwa kwa kasi, licha ya kuwa na historia ya kuwashtaki na kuwafunga viongozi wake wa zamani.