1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Rais Zelensky aomba msaada zaidi G7

13 Desemba 2022

Msimu wa baridi kali umesababisha taharuki nchini Ukraine kufuatia miundo mbinu ya nishati ya nchi hiyo kusambaratishwa na mashambulizi ya anga ya Urusi. Rais Zelensky aomba fedha za kununua gesi ya ziada

Volodymyr Zelensky
Picha: AFP/Getty Images

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amezitolea mwito nchi tajiri duniani za kundi la G7 kuipatia nchi yake gesi ya ziada pamoja na silaha ili kuisadia nchi hiyo kujinusuru na baridi kali ya msimu ambayo inatishia kusababisha mateso zaidi kwa mamilioni ya raia walioko kwenye nchi hiyo inayokabiliwa na mashambulizi ya Urusi.

Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS/REUTERS

Rais Zelensky amefanya mkutano kwa njia ya video na viongozi wa nchi tajiri kiviwanda duniani za kundi la G7  jana Jumatatu na akasema nchi yake inahitaji kiasi mita za ujazo bilioni 2 za gesi ya ziada itakayowasaidia katika kipindi hiki cha baridi kali.

Soma pia: Watu milioni 1.5 wakosa umeme huko Odessa, Ukraine

Hivi sasa nchini Ukraine theluji imetanda na mifumo yote ya nishati imesambaratishwa  na mashambulizi ya anga ya Urusi kwahivyo raia wengi wanakabiliwa na hali ya baridi kali bila ya umeme wala mifumo ya kusambaza joto majumbani mwao.

Lakini pia rais huyo wa Ukraine amewatolea mwito viongozi wa G7 kutuma silaha zaidi katika nchi yake ikiwemo vifaru vya kijeshi vya kisasa  pamoja na mizinga na makombora ya masafa marefu.

"Nawatolea mwito muongeze msaada kwa ajili ya ukraine katika suala la gesi. Ugaidi dhidi ya mitambo yetu ya umeme umetufanya tutumie kiasi kikubwa cha gesi kuliko tulivyotarajia. Na ndio sababu tunahitaji msaada zaidi katika kipindi hiki cha baridi. Tunazungumzia kiasi  mita za ujazo bilioni 2 za gesi,ambazo zinahitaji kununuliwa ziada''

Picha: Jeff J Mitchell/Getty Images

Zelensky amesema kinachochochea  alichokiita ''kiburi cha  jeshi la Urusi'' ni uwezo wa silaha walionao na huo ndio ukweli. Baadhi ya wananchi wa Ukraine kama Oleg Klyutshko mzee wa miaka 62 wanasema hawaogopi baridi kali lakini wangependelea zaidi kuona mashambulizi ya Urusi yanasitishwa na wanaweza kuvumilia hali yoyote ile.

Serikali ya Ukraine mjini Kiev inasema asilimia 40 ya miundo mbinu yake muhimu ya nishati imeharibiwa kabisa wakati mashambulizi ya Urusi yakiendelea kuilenga nchi hiyo. Wizara ya nishati ya nchi hiyo imetoa taarifa ikisema mashambulizi ya makombora ya Urusi yameharibu mitambo yake yote ya umeme unaotokana na mvuke wakati miundo mbinu yake mingine muhimu pia ikiharibiwa.

Soma pia:Urusi yazidisha mashambulizi ya angani Ukraine Mashariki 

 Kampuni ya umeme ya YASNO imesema inalazimika kuweka mgao wa usambazaji umeme katika mji mkuu Kiev ambapo kiasi asilimia 40 ya usambazaji umeelekezwa katika miundo mbinu muhimu.Lakini wakati huohuo kampuni ya mafuta na gesi ya DTEK imesema wataalamu wake wanahangaika muda wote kutafuta vifaa kukarabati miundo mbinu ya nishati iliyokwishaharibiwa na Urusi na imefikia makubaliano  na wasambazaji wa Ulaya ABB na Simens.

Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kadhalika viongozi wa kundi la G7 wamekubaliana kuhusu maeneo muhimu ya kushirikiana katika msaada wa fedha kwa ajili ya Ukraine,kwa mujibu wa  kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ambaye ameyasema hayo kabla ya mkutano wa kilele wa wafadhili wa kimataifa wa kusaidia ujenzi mpya wa Ukraine. Mkutano wa Paris unatarajiwa kuchangisha mabilioni ya dola kwa ajili ya kuwasaidia raia wa Ukraine kukabiliana na msimu wa baridi kali.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW