1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Zelensky asema ushindi utakuwa wao dhidi ya uvamizi

3 Juni 2022

Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky amesema nchi yake itaibuka mshindi na kwamba jeshi lao litaushinda uvamizi huo wa Urusi, ambao umeingia siku yake ya 100.

Ukraine | Präsident Selenskyj
Picha: John Moore/Getty Images

Akituma ujumbe mfupi kwa njia ya video kwa taifa mnamo wakati vita nchini mwake vimeingia siku 100, Zelensky amesema ana uhakika wa ushindi, licha ya mapambano makali makali kuendelea mashariki mwa nchi hiyo, ambako vikosi vya Urusi vinaimarisha udhibiti wao wa jimbo la Donbas.

Kwenye video hiyo, Zelensky anaonekana akiwa na Waziri Mkuu Denys Shmyhal na mshauri wake, Mykhaylo Podolyak, ambapo nao walikariri ujumbe na msimamo waliotangaza mwanzoni mwa uvamizi huo kwamba watasalia nchini humo.

Urusi yadhibiti karibu asilimia ishirini ya ardhi ya Ukraine

 "Kiongozi wa kikundi yuko hapa, mkuu wa ofisi ya rais yuko hapa, Waziri Mkuu wa Ukraine Shmygal yuko hapa, Podolyak yuko hapa, na rais wako yuko hapa. Timu yetu ni kubwa zaidi. Vikosi vya jeshi vya Ukraine viko hapa. Na muhimu zaidi, watu wa jimbo letu wako hapa, wakitetea Ukraine kwa siku 100 tayari. Ushindi utakuwa wetu. Utukufu kwa Ukraine," amesema Zelensky.

Wito watolewa kwa shinikizo kuongezwa dhidi ya Urusi

Mapema Ijumaa, Ukraine ilitangaza kwamba Urusi imechukua udhibiti wa moja juu ya tano ya taifa hilo ikiwemo Crimea na maeneo ya Donbas waliyomega mwaka 2014.Picha: Aris Messinis/AFP

Meya wa Kyiv alisema Ijumaa kwamba Waukraine hawataki tena siku nyingine 100 za vita, akatoa wito wa shinikizo Zaidi kuendelezwa dhidi ya utawala wa rais wa Urusi Vladimir Putin.

"Ndiyo tunahitaji silaha ili tuweze kuyalinda maadili yetu. Lakini ni sharti tuendeleze vita dhidi ya uchumi wa Urusi ili iweze kuiacha Ukraine kwa amani, ni lazima tuitenge Urusi kati ya wengine ulimwenguni,”

Wizara ya mambo ya kigeni ya Ukraine ilitoa taarifa ikisema msaada wa kimataifa kwa taifa lao, ndiyo kile ilichokitaja kuwa "uwekezaji bora zaidi kwa amani na ustawi endelevu wa kila binadamu”.

Wizara hiyo pia iliitaka mahakama maalum kuchunguza uhalifu ambao umefanywa nchini mwake ikisema wahalifu wa Urusi wanapaswa kuwajibishwa kisheria kama ilivyokuwa kwa waliokuwa viongozi wa kinazi nchini Ujerumani.

Awali, Waziri mkuu Shmyhal alisema vita hivyo vinaisogeza Ukraine karibu sana na Ulaya huku Urusi ikielekea kutengwa na ulimwengu.

Umoja wa Ulaya yatanua vikwazi dhidi ya Urusi

Umoja wa Ulaya yaiwekea Urusi vikwazo vikali vya awamu ya sita.Picha: Geert Vanden Wijngaert/AP/picture alliance

Hayo, yakijiri, nchi za Umoja wa Ulaya zimeafikiana kuridhia rasmi marufuku dhidi ya bidhaa nyingi za mafuta kutoka Urusi, hiyo ikiwa ni vikwazo vikali zaidi kwa Urusi.

Hungary yalegezewa masharti na EU iunge mkono vikwazo vya mafuta dhidi ya Urusi

Vikwazo hivyo vya awamu ya sita vimeidhinishwa na nchi zote 27 wanachama, vimelenga pia benki kubwa zaidi ya Urusi Sberbank ambayo imezuia kwenye mfumo wa kimataifa wa benki SWIFT.

Wengine waliolengwa kwenye vikwazo hivyo ni wanajeshi wa Urusi wanaotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita katika mji wa Bucha Ukraine. Na pia mchezaji wa zamani wa viungo anayedaiwa kuwa mpenzi wa rais Putin Alina Kabaeva, ambaye mali yake zitazuiwa na visa yake kuwekewa vikwazo.

(AFPE, RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW