1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Zelensky asifu mafanikio ya jeshi la Ukraine

7 Agosti 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelisifu jeshi la nchi yake kwa kuendesha operesheni kabambe za kujibu mapigo dhidi ya vikosi vya Urusi.

Russische Militäraktion in der Ukraine
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/ZUMA/IMAGO

Akizungumzia kupitia ujumbe wa vidio wa kila siku alioutoa siku ya Jumamosi, Zelensky amesema katika kipindi cha wiki moja iliyopita, jeshi la Ukraine limepata mafanikio makubwa kwa kuharibu mikakati ya jeshi la Urusi.

"Kila shambulizi kwenye maghala ya silaha ya adui, kwenye vituo vyao vya operesheni na dhidi ya vifaa vyao vya kijeshi linanusuru Maisha ya sisi sote, maisha ya wanajeshi wa Ukraine na raia” amesema Zelensky.

Zelensky alikuwa akizungumzia mafanikio madogo ambayo jeshi la nchi hiyo limeyapata kwenye majimbo ya Kherson na Zaporizhzhia yaliyokamatwa na Urusi miezi ya hivi karibuni.

Vikosi vya Ukraine vimemudu kuyakomboa baadhi ya maeneo lakini sehemu kubwa ya majimbo hayo bado yanadhibitiwa na Urusi.

Zelensky awashukuru washirika wa magharibi kwa msaada wa silaha 

Kiongozi huyo pia amegusia mchango mkubwa uliotokana na msaada wa silaha kutoka mataifa washirika. Ametoa shukrani kwa mataifa ya magharibi kwa kuipelekea silaha nchi yake.

Zelensky pia ameishukuru mahsusi Marekani baada ya taifa hilo kutangaza kuwa litaipatia Ukraine msaada mwingine wa silaha zenye thamani ya dola milioni 550.

Picha: Sofiia Gatilova/REUTERS

Hata hivyo duru kutoka mjini Washington zinasema msaada huo unaweza kufikia dola bilioni 1 za Marekani. Huo utakuwa msaada mkubwa wa kijeshi kuwahi kutolewa, na utajumuisha makombora na magari ya kisasa ya kijeshi kwa ajili ya matibabu.

Tangazo la msaada huo linatarajiwa kutolewa mapema wiki ijayo na itakuwa ni nyongeza kwa msaada wa dola bilioni 8.8 ambazo tayari Marekani imeipatia Ukraine tangu Urusi ilipoivamia kijeshi nchi hiyo mnamo Februari 24.

Maafisa waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina wamesema hata hivyo,  rais Joe Biden wa Marekani bado hajatia Saini awamu hiyo mpya ya msaada kwa Ukraine.

Hofu yaongezeka baada ya kuripotiwa uharibu kwenye kinu cha nyulkia 

Katika hatua nyingine rais Zelensky ameituhumu Urusi kwamba inatumia kituo cha kufua umeme kwa nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kwa malengo ya "kigaidi" baada ya waendeshaji wa kituo hicho kuripoti kuwa kumetokea uharibifu mkubwa.

Kinu cha nyuklia cha kufua nishati ya umeme cha Zaporizhzhia Picha: Dmytro Smolyenko/Ukrinform/IMAGO

Kampuni ya Energoatom, inayoendesha kituo cha kufua umeme cha Zaporizhzhia kilicho kusini mwa Ukraine, imeripoti siku ya Jumamosi kwamba sehemu ya kinu hicho "imeharibiwa vibaya” na mashambulizi ya kijeshi na mtambo mmoja wa nyuklia umelazimika kuzimwa.

Ukraine na Urusi kila upande unamlaumu mwingine kuhusika na mashambulizi hayo dhidi ya kinu hicho ambacho ndicho kikiubwa zaidi barani Ulaya.

Rais Zelensky ameituhumu Urusi akisema "magaidi wa kirusi wamekuwa wa kwanza duniani kutumia kituo cha kufua umeme kwa malengo ya kigaidi"

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell  amelaani mashambulizi hayo akiyataja kuwa "ukiukaji mkubwa wa kanuni za usalama wa nishati ya nyuklia na mfano mwingine- wa jinsi Urusi inavyopuuza desturi za kimataifa"

Mkuu wa shirika la Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA, Rafael Grossi, ameelezea wasiwasi juu ya taarifa za kulengwa kwa kinu hicho akisema hujuma hizo zinaonesha wazi kitisho cha kutokea janga la nyuklia.

IAEA pia imetaka kupatiwa nafasi ya wataalamu wake kukifikia kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kwa ajili ya ukaguzi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW