1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Zelensky aulilia Ulimwengu

25 Februari 2022

Rais Zelensky aulalamikia ulimwengu kwa kukaa tu na kuendelea kutazama kinachoendelea ndani ya Ukraine

Ukraine-Konflikt - Präsident Selenskyj
Picha: Ukrainian President's Office/ZUMA Press/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Ijumaa kwamba uchokozi wa Urusi unaoendelea dhidi ya nchi yake umeonesha kwamba vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi havitoshi. Hali bado inazidi kuwa ya mashaka nchini Ukraine ambako wananchi wake wanaendelea kukimbia.

Akizungumza mapena hii leo Ijumaa, Rais Zelensky ameualalamikia ulimwengu kwa kukaa tu na kuendelea kutazama kinachoendelea ndani ya Ukraine, baada ya mji mkuu Kiev na maeneo mengine ya nchi hiyo kushambuliwa kwa makombora na Urusi majira ya asubuhi ya leo.

Picha: Ukrainian President's Office/ZUMA Press/picture alliance

"Asubuhi hii tuko peke yetu katika kuitetea nchi yetu kama ilivyokuwa jana. Vikosi vya majeshi yenye nguvu zaidi duniani vinatutazama kutokea mbali. Je vikwazo vya jana viliishawishi Urusi? Tunayoshuhudia  angani na kuyapitia yale yanayojitokeza ardhini yanaonesha kwamba vikwazo havikutosha."

Hotuba ya Rais Zelensky aliyoitowa kupitia televisheni ilikuwa ikiwalenga Warusi  akisema mashambulizi yanayofanywa na nchi hiyo dhidi ya Kiev ni sawa na yale yaliyofanywa na Wanazi wa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Shirika linalohusika na masuala ya nyuklia la Ukraine limesema kwamba hii leo viwango vya mionzi ya nyuklia vimeongezeka kutoka eneo la mtambo usiotumika  wa kuzalisha umeme wa  nyuklia wa Chernobyl.

Picha: Czarek Sokolowski/AP/picture alliance

Aidha washauri wa Rais Volodymyr wamesema bado kiongozi huyo wa Ukraine yupo katika mji mkuu Kiev na hajaondoka. Shirika la habari la Urusi, RIA, likinukuu ripoti za shirika la habari la Associeted Press limefahamisha kwamba milio ya risasi imesikika karibu na eneo la majengo ya shughuli za kiserikali katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev.

Mshauri wa serikali ya Ukraine amesema huenda Urusi ikajaribu kuingia Kiev hii leo na wakaazi wa mji huo wametolewa mwito kuendelea kukimbilia maeneo ya kujihifadhi  kufuatia tahadhari za mashambulizi ya anga zinazotolewa.

Yote haya yanajitokeza huku viongozi wa nchi za Magharibi wakipanga kukutana kwa dharura kuzungumzia yaliyojiri na Rais Zelensky akiitolea mwito jumuiya ya kimataifa kuisadia nchi yake kuzuia mashambulizi ya Urusi ambayo yanaweza kuipindua madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, kusababisha maafa makubwa na pia kuleta athari kubwa za kiuchumi duniani.

Picha: Sefa Karacan/AA/picture alliance

Dalili zinazoonesha kwamba kuna kitisho kikubwa cha mji mkuu Kiev kuvamiwa na Urusi ni kuonekana kwa kundi la majasusi wa Kirusi kiasi kilomita tano kutoka mjini Kiev.

Umoja wa Ulaya unataka kufuta mafungamano yote baina ya Urusi na mifumo yote ya fedha ya dunia kwa mujibu wa waziri wa fedha wa Ufaransa.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, kwa upande mwingine, atafanya mazungumzo na maafisa wa majimbo yaliyojitangazia uhuru  ya Donetsk na Luhansk ya mashariki mwa Ukraine baadae hii leo

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW