1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raisi aonya waandamanaji nchini Iran

23 Septemba 2022

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema jana kwamba matukio ya vurugu hayakubaliki, huku akiwaonya waandamanaji walioingia mitaani kote nchini humo kuelezea ghadhabu zao dhidi ya kifo cha Mahsa Amini.

Iran
Picha: Iranian Presidency Office/AP/picture alliance

Msichana huyo wa miaka 22 alikuwa akizuiwa kwenye kituo cha polisi wa maadili nchini humo. 

Alipozungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, rais Ebrahim Raisi amesema tayari ameagiza kufanyika uchunguzi wa tukio hilo la Mahsa aliyefariki wiki moja baada ya kukamatwa kwa madai ya kuvaa mavazi yasiyokubalika.

Alinukuliwa akisema kuna uhuru wa kujieleza Iran, lakini vitendo vya vurugu havikubaliki.

"Bila shaka, haya ni ya kawaida na yaliyotarajiwa kabisa, lakini ni lazima tutofautishe kati ya waandamanaji na waharibifu. Maandamano ni mazuri kwa sababu watu fulani wanaweza kuwa na maoni ambayo wangependa kuyatoa kuhusu masuala mahususi. Kuna mambo leo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mambo ambayo yanajadiliwa, mambo ambayo ndani yake kuna maoni mengi tofauti." alisema Raisi.

Aidha kiongozi huyo amesisitiza kwamba Amini hakuteswa na polisi, ingawa amesema, bado analifuatilia na iwapo kulikuwepo na mapungufu ni lazima kutafanyika uchunguzi.

Wanawake wakiwa wameshika picha ya Mahsa Amini aliyekufa baada ya kuzuiwa na polisi wa maadili .Picha: Bilal Hussein/AP/picture alliance

Kwa upande mwingine, Raisi ameyatuhumu mataifa ya magharibi kwa undumila kuwili na kuchochea hali ya wasiwasi na hasa baada ya kuiwekea vikwazo idara hiyo ya kipolisi, huku akinyooshea kidole mauaji yanayofanywa na polisi nchini Marekani na vifo vya wanawake nchini Uingereza.

Kikosi cha Walinzi wa Kimapinduzi chenye ushawishi mkubwa nchini Iran kimeitolea mwito mahakama kuwashitaki wote wanaosambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii na mitaani, likisema wanahatarisha usalama wa kisaikolojia wa jamii, na kuitaka mahakama kuwakabili ipasavyo.

Mkuu wa mahakama Gholamhossein Mohsein Ejei ameagiza kuendeshwa haraka kwa kesi za waandamanaji ili kuimarisha usalama na amani kwa raia.

Wizara ya intelijensia ya Iran pia imejaribu kuyazuia maandamano hayo ikionya ni kinyume cha sheria kushiriki kwenye maandamano na yoyote anayeandamana atafunguliwa mashitaka, hii ikiwa ni kulingana na tovuti za habari za Iran.

Haya ni maandamano makubwa kabisa kushuhudiwa kwenye taifa hilo la Kiislamu tangu mwaka 2019, huku wanawake waliojitokeza kwa kiasi kikubwa wakichoma moto hijabu zao.

Sikiliza Zaidi: 

22.09.2022 Matangazo ya Jioni

This browser does not support the audio element.

Kifo cha Amini kimechochea ghadhabu dhidi ya masuala ambayo ni pamoja na vizuizi katia uhuru binafsi nchini Iran ikiwa ni pamoja na mavazi kwa wanawake na uchumi uliozoroteshwa na vikwazo. Viongozi wa dini wanahofia kurejea kwa maandamano makubwa kabisa kama ya mwaka 2019 yaliyoibuka baada ya kuongezeka kwa gharama za gesi ambapo mamia ya waandamanaji waliuawa.

Mashirika: RTRE/AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW