1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Imani

Ramadhan na Kwaresima: Misimu mikuu ya Kiroho

18 Februari 2026

Kwa mara ya kwanza baada ya takriban miaka 30, Waislamu na Wakristo katika sehemu mbalimbali za dunia wanaanza kwa wakati mmoja misimu yao mikuu ya kiroho — Ramadhan na Kwaresma.

Waislamu katika ibada ya kuanza kwa Ramadhan Jeddah(kushoto)-muumini wa Kikristo katika ibada ya Jumatano ya majivu(kulia)
Picha mbili zinazoonyesha Waumini wa Kiislamu mjini Jeddah na muumini wa Kikristo katika ibada ya Jumatano ya majivuPicha: Mohammed Zarandah/Anadolu Agency/IMAGO/Matthias Bein/dpa/picture alliance

Wakati Waislamu wakianza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, Wakristo nao wanaanza kipindi cha siku 40 cha Kwaresma kwa maombi, toba na tafakari. Lakini mwaka huu, sherehe na ibada hizi zinafanyika katika mazingira tofauti — baadhi ya maeneo yakiwa katika vita, huku waumini wakitafuta amani na matumaini.

Mamilioni ya Waislamu duniani wanaanza kufunga kuanzia alfajiri hadi machweo, wakiadhimisha mwanzo wa mwezi wa Ramadhan — mwezi wa ibada, tafakari na kutoa sadaka. Nchini Saudi Arabia, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu na baadhi ya mataifa ya Afrika, Ramadhan imeanza Jumatano baada ya kuandama kwa mwezi mwandamo, huku mataifa mengine ya dunia ikitarajiwa kuanza Alhamisi kutokana na tofauti za uangalizi wa mwezi.

Maandalizi ya Ramadhani huko Yerusalemu MasharikiPicha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Hali katika Ukanda wa Gaza

Katika Ukanda wa Gaza, Ramadhan inaanza katika mazingira magumu ya vita. Mashambulizi ya kijeshi yamesababisha vifo vya maelfu ya Wapalestina na uharibifu mkubwa wa makazi. Hata hivyo, matumaini bado yanaonekana miongoni mwa wakazi.

Msanii wa Kipalestina, Yazeed Abu Jarad, alichora maneno ya "Karibu Ramadan” kwenye mchanga wa pwani ya Deir el-Balah kama ishara ya matumaini na kuongeza kuwa "tunaiambia dunia yote kwamba bado tunaendelea vizuri, na tunatumaini kuwa Ramadhani hii itakuwa huru bila vita na mashambulizi ya mabomu. Tumekuwa vitani kwa miaka mitatu, Ramadhani zetu zote zimekuwa katikati ya vita, lakini tunamuomba Mungu isiwepo tena vita.”

Kuanza kwa mfungo wa Kwaresima

Wakati huo huo, mamilioni ya Wakristo kote duniani wameadhimisha Jumatano ya Majivu kuanza kwa kipindi cha Kwaresma. Kipindi hiki cha siku 40 ni cha toba, maombi na tafakari juu ya mateso na ufufuo wa Yesu Kristo.

Mfanano wa ibada ya funga kati ya Waislamu na Wakristo

02:18

This browser does not support the video element.

Miongoni mwa waumini waliohudhuria ibada jijini Manila ni Marie Blancaflor mwenye umri wa miaka 48. "Hii ndiyo namna tunaweza kujitambulisha kwa Bwana na kuelewa sadaka yake, hivyo katika siku hizi 40 zijazo tunapaswa kujichunguza kuhusu matendo yetu, dhambi zetu na sadaka ya Mungu."

Licha ya tofauti za kidini na kijiografia, Ramadhan na Kwaresma mwaka huu zinakutana katika ujumbe mmoja wa pamoja — kufunga, kuomba na kutafakari. Katika dunia yenye migogoro na changamoto nyingi, waumini wa dini hizi mbili wanatumia kipindi hiki kuombea amani, msamaha na matumaini mapya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW