1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RAMALLAH : Abbas kutaka yakinisho kutoka kwa Bush

22 Mei 2005

Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas amesema leo hii atamshinikiza Rais George W Bush wa Marekani kupatiwa msaada wa kisiasa na kiuchumi pamoja na ufafanuzi juu ya namna Marekani itakavyofuatilia utekelezaji wa amani ya Mashariki ya Kati baada ya Israel kujitoa katika Ukanda wa Gaza.

Rais Abbas ambaye anaelekea Washington katika ziara yake ya kwanza rasmi katika Ikulu ya Marekani hapo Alhamisi ametowa kauli hiyo baada ya kurudi katika mikutano na viongozi wa dunia ikiwa ni pamoja na Rais Hosni Mubarak wa Misri.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah Abbas amesema atamtaka Bush aweke wazi msimamo wa Marekani juu ya utekelezaji wa mpango wa amani baada ya kujiondoa kwa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Wapalestina wanataka kuanza tena mazungumzo ya amani yaliokwama yanayodhaminiwa na Marekani ambayo yanataka kuundwa kwa taifa la Palestina katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza ardhi ambazo zimetekwa na Israel katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967.