1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RAMALLAH: Mshauri wa rais Abbas ajiuzulu

26 Julai 2007

Mshauri wa usalama wa kitaifa wa rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, amejiuzulu hii leo. Rais Abbas amelikubali ombi la kujiuzulu kwa Mohammed Dahlan mwenye umri wa miaka 46, ambaye pia alishikilia wadhifa wa katibu katika baraza la usalama wa kitaifa ambalo lilivunjwa na rais Abbas hivi majuzi.

Dahlan, mbunge wa chama cha Fatah cha rais Abbas na ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa katika Ukanda wa Gaza, amekuwa msitari wa mbele kupinga kundi la wanamgambo wa kiislamu la Hamas.

Ofisi ya Dahlam imesema amejiuzulu kwa sababu za kiafya na hivi sasa anatibiwa katika Yugoslavia ya zamani kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita kwenye goti lake.

Duru zilizo karibu na Dahlan zinasema wamekubailna na rais Abbas kuhusu kujiuzulu kwake na bado wana mawasiliano ya karibu.

Dahlan bado anaongoza kamati inayoshughulikia maswala ya ndani na usalama ya baraza la bunge la Palestina.