1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa ahimiza "mshikamano wa mataifa" mkutano wa G20

22 Novemba 2025

Mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi duniani la G20 umefunguliwa rasmi siku ya Jumamosi mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Afrika Kusini Johannesburg 2025 | Rasi Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akifungua mkutano wa G20
Rasi Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akifungua mkutano wa G20 unaofanyika mjini Johannesburg.Picha: Jerome Delay/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika chini ya kiwingu cha kutohudhuriwa na viongozi wengi wa dunia na mjadala mkali kuhusu mpango wa Marekani wa kumaliza vita vya Ukraine.

Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na viongozi wa Urusi na China - Vladimir Putin na Xi Jinping - ni miongoni mwa viongozi waliositisha mipango ya kushiriki mkutano huo wa G20 unaofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Viongozi wa Mexico na Argetina pia hawahudhuria mkutano huo huku Rais Bola Tinibu wa Nigeria amelazimika kuifuta safari yake ya kwenda kushiriki mkutano huo ili kushughulia mkasa wa kutekwa wanafunzi zaidi ya 300 na makundi ya watu wenye silaha kaskazinji mwa nchi yake.

Utawala wa Trump umesusia mkutano huo kwa sababu unaituhumu serikali ya Afrika Kusini kwa kufanya ukandamizaji dhidi ya jamii ya wazungu wachache wa nchi hiyo.

Afrika Kusini imekanusha madai hayo ikisema haya msingi wala ushahidi.

Mwenyeji wa mkutano huo wa kilele wa G20, Rasi Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini anatoa kipaumbele kwa mada za mshikamano, usawa na maendeleo endelevu.

Amesema atatumia mkutano huo kupigia debe kupunguzwa mzigo wa madeni kwa mataifa yanayoendelea, usawa katika kuhamia kwenye nishati safi zisizoharibu mazingira, matumizi ya haki ya madini adimu, upatikanaji chakula na mgawanyo wa haki wa majukumu ya kulinda mazingira duniani.

Macron, Modi na Lula washiriki mkutano wa G20

Rais Donald Trump wa Marekani ameususia mkutano wa G20 unaofanyika Afrika Kusini.Picha: Ercin Erturk/Anadolu/picture alliance

Viongozi wa G20 wamekusanyika kwenye kituo cha maonesho kilichobadilishwa kuwa ukumbi karibu na mji wa Soweto, eneo alikoishi wakati fulani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Waziri Mkuu Narendra Modi wa India, Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na Waziri Mkuu wa China Li Qiang ni miongoni mwa wale wanaohudhuria.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais Cyril Ramaphosa amelimpiga kijembe Trump kwa kusisitiza umuhimu wa "mataifa kufanya kazi pamoja" kushughulikia changamoto za dunia badala ya kuendekeza mivutano.

Amesema pia mkutano huo utakaomalizika siku ya Jumapili umefanikiwa kupata azimio licha ya upinzani kutoka Marekani.

Hapo jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres aliwatolea mwito viongozi wa G20, kutumia ushawishi wao kumaliza mizozo duniani ambayo imekuwa chanzo cha vifo, uharibifu na kukosekana uthabiti kote ulimwenguni.

Mkwamo kwenye mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi katika mkutano wa COP 30 unaofanyika Belem Brazil ni mojawapo ya masuala yatakayotia kiwingu mkutano wa G20.

Mkutano huo uliopaswa kukamilika Ijumaa jioni umerefushwa kuruhusu majadiliano zaidi kati ya pande zinazokinzana.

Msuguano mkubwa upo kwenye kuandaa azimio la mwisho baada ya wawakilishi wa nchi zinazoendelea kutaka kuwemo kipengele kinachoshinikiza kupunguzwa uzalishaji na matumizi ya nishati za visukuku.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW