Ramaphosa asema mkutano wa G20, Afrika Kusini ulifanikiwa
24 Novemba 2025
Viongozi wa nchi zilizoshiriki kukubaliana juu ya tamko la pamoja linalozungumzia kwa kina masuala muhimu ya kimataifa, hatua ambayo inaonyesha kwamba licha ya tofauti zao, bado wameweza kufikia mwafaka kuhusu mambo ya msingi kwa mustakabali wa dunia.
Tamko hilo, lililokubaliwa na mataifa 19 yaliyoshiriki, liliweka mbele ajenda za dharura za dunia, ikiwemo mzozo wa tabianchi na msaada kwa nchi zilizo hatarini kukumbwa na majanga ya hali ya hewa. Pia liliangazia pengo la usawa duniani, likiwemo suala la urejeshaji upya wa mifumo ya madeni. Rais Cyril Ramaphosa amesema tamko hilo linatoa wito wa kupatikana kwa amani ya haki nchini Ukraine, Palestina na Sudan.
''Kupitishwa kwa tamko hilo ni ujumbe mzito kwa dunia kwamba ushirikiano wa kimataifa bado unaweza kuzaa matokeo, na ni ishara ya matumaini na mshikamano duniani.''
Naye Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen aliibua changamoto za maendeleo barani Afrika.
''Licha ya dunia kuwekeza zaidi ya dola trilioni mbili katika nishati safi mwaka uliopita, Afrika imenufaika kwa asilimia mbili tu, wakati ina watu milioni 600 wasio na umeme, lazima tubadilishe uwiano huu.''
Trump asusia mkutano wa G20
Hata hivyo, Marekani ilipinga kutolewa kwa tamko hilo bila mchango wake, ikilitaja kuwa hatua ya aibu. Rais Donald Trump alisusia mkutano huo, akiilaumu Afrika Kusini "kuwatendea vibaya watu wachache weupe", na pia kutokana na upinzani wake dhidi ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutatua pengo la ukosefu wa usawa duniani.
Kutokana na kukosekana kwake, Afrika Kusini iligoma kumkabidhi kijiti cha uongozi wa kundi la mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani, G20 kaimu balozi wa Marekani humu nchini, David Green.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, alieleza kuwa sherehe ya makabidhiano ya uenyekiti katika mkutano wa G20 ingehitaji uwepo wa maafisa wa ngazi ya juu na siyo balozi na sasa yatafanyika katika ofisi za mambo ya nchi za nje ya afrika Kusini.
Kipi kinafuata baada ya mkutano?
Licha ya kususiwa na Marekani, viongozi kutoka India, Kanada, Brazil, Umoja wa Ulaya na wanachama wengine walihudhuria na walikubaliana wote kwa pamoja maazimio yote. Je, hatua inayofuata kwa G20 ni ipi? Chimbizga Msimko ni mchambuzi wa siasa, nimezungumza naye akiwa Lilongwe, Malawi:
"Makubaliano ya G20 hayalazimishi, hivyo yanabaki kuwa matamko ya nia badala ya sheria zinazotekelezeka moja kwa moja. Kutokana na Marekani kutoyaridhia, ina nafasi ya kutojumuika katika utekelezaji wa baadhi ya vipengele muhimu, kama kufadhili miradi ya mabadiliko ya tabianchi au kuunga mkono mageuzi ya mifumo ya kifedha ya kimataifa. Hali hii inaweza kusababisha maazimio ya mkutano kutekelezwa kwa kiwango kidogo au kwa upande mmoja tu, jambo linalopunguza nguvu na ushawishi wa jumla wa makubaliano hayo."
G20 inawakilisha asilimia 85 ya uchumi wa dunia na takribani theluthi mbili ya watu wote duniani. Ilianzishwa mwaka 1999 kufuatia msukosuko wa kifedha barani Asia, na ikaimarishwa zaidi baada ya mdororo wa uchumi wa dunia wa mwaka 2008.
Upana wake na wigo mkubwa wa wanachama vilionekana kuwa njia bora zaidi ya kukabili migogoro kuliko kutegemea kundi dogo la G7.