1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa ataka uhalifu kushughulikiwa kikamilifu

Bryson Bichwa
13 Februari 2026

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametuma vikosi vya wanajeshi kushirikiana na polisi kukabiliana na wimbi la uhalifu wakati kukiwa na ongezeko la matukio ya uporaji, ujambazi na shughuli haramu za uchimbaji madini.

Zimbabwe SADC Treffen in Harare
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Picha: Jekesai Njikizana/AFP

Katika hotuba yake kwa Taifa, maarufu kama SONA 2026, Rais Cyril Ramaphosa alisisitiza kuwa serikali haitavumilia uhalifu unaovuruga uchumi na kuhatarisha maisha ya raia. Aliahidi kuwa operesheni maalum zitafanyika kulenga makundi yanayojihusisha na uchimbaji haramu wa madini, maarufu kama zama zama:

"Nitapeleka Jeshi la Ulinzi la Taifa la Afrika Kusini (SANDF) kusaidia polisi, kama tulivyofanya kwa mafanikio makubwa katika kukabiliana na uchimbaji haramu wa madini. Nimemuelekeza Waziri wa Polisi pamoja na Jeshi kuandaa mpango wa kitaalamu utakaoainisha maeneo ambayo vikosi vitapelekwa katika siku chache zijazo katika Western Cape na Gauteng, kwa lengo la kukabiliana na vurugu za magenge na uchimbaji haramu."

Rais Ramaphosa pia alitoa onyo kali kwa wananchi dhidi ya vitendo vya kujichukulia sheria mkononi vinavyolenga raia wa kigeni akisema nchi yake haitovumilia matendo ya vurugu na uvunjifu wa sheria utakaofanywa na mtu yeyote yule.

"Hatutavumilia vurugu wala matendo ya uvunjifu sheria yanayolenga raia wa kigeni. Hakuna raia wa kigeni anayepaswa kuzuiawi kutumia huduma za umma, ikiwa ni pamoja na vituo vya afya na shule."

Malema apongeza tangazo la rais

Miongoni mwa waliopokeza hotuba hiyo kwa msukumo mkubwa ni kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters, Julius Malema:

Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters, Julius Malema.Picha: Guillem Sartorio/AFP

"Tunafurahia kuwa jeshi linaingia. Tutaweka sheria na utulivu kwa usahihi. Mambo mengine yote anayozungumzia si mapya kwake, amekuwa akiyazungumza tokea hapo awali. Tofauti ya leo ni kwamba anazungumza kwa nguvu na msukumo mkubwa."

Mkaazi wa Pretoria, Ezekiel Ndundu, pia ameguswa na hotuba ya Rais:

"Cyril Ramaphosa ni kiongozi msomi. Hii tabia ya kuhakikisha watoto wa wageni wanaweza kwenda shule za umma, inaonyesha sura nzuri ya nchi kimataifa.''

Kabla ya kuanza kwa hotuba, wanachama wa EFF walionekana wakiimba na kuonyesha umoja wao nje ya ukumbi wa Bunge, ishara ya uwezekano wa mijadala mikali. Hata hivyo, hadi hotuba ilipoanza, hali ya usalama ilikuwa imedhibitiwa huku vyombo vya dola vikiwa vimeimarisha ulinzi ndani na nje ya ukumbi hapa Cape Town.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW