1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa: Ghasia zilipangwa

Lilian Mtono
16 Julai 2021

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema kwamba machafuko na ghasia zilizojitokeza nchini humo zilikuwa ni za kupangwa. Watu takriban 117 wamekufa kufuatia machafuko hayo.

Südafrika | Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: Esa Alexander/Pool/REUTERS

Rais Ramaphosa amesema hayo alipotembelea manispaa ya Ethekwini inayojumuisha mji wa bandari wa Durban, ambao ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa pakubwa na ghasia za wiki iliyopita pamoja ya matukio ya uporaji na moto ulioharibu biashara nyingi na kusababisha vifo vya watu 100. Kulingana na mamlaka, watu 12 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na machafuko hayo yaliyochochewa na hukumu ya kifungo ya rais wa zamani Jacob Zuma.

Aidha ameelezea wasiwasi kuhusiana na kuongezeka kwa mivutano yenye mwelekeo wa ubaguzi wa rangi katika baadhi ya maeneo nchini humo. Baadhi ya maeneo yanayokaliwa na wazungu walio wachache na jamii ya Wahindi ambao kwa kawaida huwa na maisha mazuri kuliko weusi, wamekuwa wakijihami kwa silaha ili kujilinda na waandamanaji.

Amenukuliwa akisema ni wazi matukio hayo yalipangwa na ni shambulizi dhidi ya demokrasia na kuongeza kuwa kulikuwa na watu walioyapanga na kuyaratibu. Na kufuatia hali hiyo, Ramaphosa akasisitiza kuhusiana na suala la kupeleka wanajeshi zaidi huku akilaani vikali ghasia hizo.

"Hiki sicho tunachotaka kukishuhudia nchini mwetu na ni wazi kwamba tunatakiwa kuchunguza upya kila tunachokifanya katika kuwalinda watu wetu na mali zao. Lakini kwa sasa, ninapenda kusema tunapeleka vikosi vya usalama. Wanajeshi 25,000 tayari wanasambazwa, na baada ya muda mfupi watakuwa kwenye jimbo zima la KwaZulu Natal na mengineyo kama Gauteng," alisema Ramaphosa. 

Polisi wakisaidia kukusanya bidhaa zilizoporwa kwenye moja ya maduka nchinI Afrika Kusini.Picha: Luca Sola/AFP

Ramaphosa amesema akiwa kwenye jimbo la nyumbani la Jacob Zuma la Kwa-Zulu Natal kwamba wahusika wametambuliwa na kwamba taifa hilo halitaruhusu kuibuka kwa machafuko na matukio ya uchomaji moto kutokea na kukiri kwamba wangetarajia kufanya vizuri zaidi, lakini walikuwa wameelemewa na mazingira yaliyokuwepo. Hata hivyo ameahidi serikali yake kufanya kila linalowezekana kukabiliana na ghasia ambazo amesema zimeathiri pakubwa uaminifu wa wawekezaji, lakini pia hatua za kuuimarisha tena uchumi wa taifa hilo.

Huku akisema hayo, kumeripotiwa ongezeko la hali ya wasiwasi ya usambazaji wa bidhaa muhimu nchini Afrika Kusini.

Kulingana na maafisa, idadi rasmi ya vifo imefikia 91 katika jimbo la KwaZulu Natal na 26 katika jimbo la Gauteng, linalojumuisha mji wa Johannesburg na kufanya idadi jumla kufikia 117. Mawaziri wa ulinzi, usalama na polisi pamoja na majenerali wa ngazi za juu wako KwaZulu Natal tangu jana Alhamisi kutathmini hali na kusimamia usambazaji wa wanajeshi wa usalama.

Soma Zaidi: Maoni: Machafuko Afrika Kusini yafichua kushindwa kwa serikali

Mashirika: AFPE/APE/RTRE