1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa kuapishwa rais mpya wa Afrika Kusini

15 Februari 2018

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC kimesema bunge litamchagua na kumuapisha makamu wa rais Cyril Ramaphosa kuwa rais mpya wa taifa hilo hii leo muda mfupi tu baada ya rais Jacob Zuma kutangaza rasmi kujiuzulu.

Südafrika Cyril Ramaphosa in Johannesburg
Picha: picture-alliance/Photoshot

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress, ANC kimesema bunge litamchagua na kumuapisha makamu wa rais Cyril Ramaphosa kuwa rais mpya wa taifa hilo hii leo, muda mfupi tu baada ya rais Jacob Zuma kutangaza rasmi kujiuzulu wadhifa huo, kufuatia siku kadhaa za shinikizo la kutakiwa kujiuzulu kutoka ndani ya chama chake kutokana na tuhuma za rushwa, kuporomoka kwa uchumi wa taifa hilo na kuharibu sifa ya chama hicho.

Cyril Ramaphosa sasa anatarajiwa kuchaguliwa na hatimaye kuapishwa na bunge majira ya saa 8 mchana kwa saa za Afrika Kusini hii leo, taarifa hii ikiwa ni kulingana na mnadhimu mkuu wa chama tawala cha ANC bungeni, Jackson Mthembu. 

Mthembu amekieleza kikao cha kamati ya bunge kwamba, ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali imesema iko tayari kusimamia shughuli hiyo ya kumpata rais mpya.  

Kwenye kikao hicho pia, spika wa bunge alisema barua ya kujiuzulu ya Jacob Zuma mwenye miaka 75 aliyetangaza maamuzi hayo usiku wa jana Jumatano kwenye hotuba aliyoitoa kupitia televisheni, ili kuepuka kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye itawafikia baadae.

Rais Jacob Zuma anaondoka madarakani huku akikabiliwa na tuhuma lukuki za ufisadi Picha: picture-alliance/dpa/EPA/A. Ufumeli

Kwenye hotuba hiyo, Zuma pamoja na kutangaza maamuzi hayo alitoa malalamiko dhidi ya chama chake akidai kwamba kilimtishia kumuondoa kwa kura ya bunge ya kutokuwa na imani naye, akikitaka chama hicho kumpa sababu za kumshinikiza kuachia madaraka hayo mara moja.

Alisema kwenye hotuba yake ya awali kupitia televisheni hapo jana, akishutumu hatua zinazochukuliwa na  chama chake cha ANC kumuondoa madarakani kuwa si za haki. Alijiunga na chama hicho mwaka 1959.

Zuma alalama dhidi ya hatua zinazochukuliwa dhidi yake na chama chake mwenyewe.

Alisema amechukizwa na namna ambavyo hatua hizo zimekuwa zikitekelezwa. alisema hakubaliani nazo na hakuna uthibitisho unaoonyesha iwapo amefanya ovu lolote.

Zuma alisema kwenye hotuba hiyo kwamba "ninalazimika kukubali kwamba iwapo chama changu na washirika wenzangu wanataka niondolewe madarakani, wanatakiwa kulifanya hilo kwa haki, kwa kuzingatia namna katiba inavyoelekeza".

Kuliongezeka na shinikizo katika siku za karibuni kumtaka Zuma kung'oka.Picha: picture-alliance/T.Hadebe

Kamati kuu ya ANC ilimtaka Zuma kuachia madaraka siku ya Jumanne, baada ya kikao cha masaa 13, nje kidogo ya mji wa Pretoria, lakini alikataa. 

Baadhi ya raia nchini humo wameelezea kujiuzulu kwa Zuma kama hatua muhimu ya kuimarisha umoja na hali ya uchumi nchini humo, kama mwanafunzi huyu Phumza Mjilana anavyosema.

Hata hivyo, naibu katibu mkuu wa ANC Jesse Duarte alisikika baada ya hatua hiyo ya Zuma ya kujiuzulu akisema "hatushangilii". Aliongeza kuwa "tulilazimika kumuondoa mtu aliyekuwa muhimu kwenye vuguvugu ndani ya ANC kwa zaidi ya miaka 60, hili si suala dogo".  

Jana asubuhi, polisi walivamia makazi ya familia ya wafanyabiashara matajiri waliokuwa na ushawishi mkubwa kwenye serikali ya Zuma ya Gupta, ambao pia wanahusishwa kwenye tuhuma za kifisadi zilizomkabili kiongozi huyo wakati wa utawala wake. 

Ramaphosa mwenye miaka 65, anayechukua madaraka kutoka kwa Zuma, anakabiliwa na changamoto ya kufufua uchumu na kupambana na uwozo wa ufisadi serikalini. Ni mshirika wa zamani wa Nelson Mandela aliyeongoza mazungumzo ya kumaliza utawala wa kibaguzi mapema miaka ya 1990, na baadaye kuwa mfanyabiashara mkubwa kabla ya kujiunga na siasa.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Iddi Ssessanga 


 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW