1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuteuliwa kwa Ramaphosa kumemuweka katika hali ngumu

Amina Abubakar 20 Desemba 2017

Cyril Ramaphosa anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza kama rais wa chama tawala cha African Nationa Congress ANC nchini Afrika kusini

Südafrika Cyril Ramaphosa in Johannesburg
Picha: picture-alliance/Photoshot

Ramaphosa, ambaye pia ni makamu wa rais wa Afrika Kusini na mfanyabiashara tajiri, alimshinda mpinzani wake Nkosazana Dlamini Zuma aliyekuwa Waziri wa afya na mtalaka wa Rais Jacob Zuma kwa ushindi mdogo katika kuwania nafasi hiyo ya juu katika chama tawala ANC.

Ushindi wake ulishusha pumzi za wengi wa wanachama wa chama hicho, wanaoamini Ramaphosa atakuwa hewa safi katika chama hicho kilichokumbwa na madai chungu nzima ya rushwa wakati wa mihula miwili ya utawala wa rais Jacob Zuma.

Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: picture-alliance/AP Photo/T.Hadebe

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanasema kuteuliwa kwa Ramaphosa, mwenye umri wa miaka 65, kumemuweka katika hali ngumu kwasababu nafasi zote kubwa za uongozi makamu wa rais wa chama cha ANC zimewaendea wale wanaomuunga mkono Rais Jocob Zuma.

Gary van Staden mchambuzi nchini Afrika Kusini amesema Cyril Ramaphosa atakuwa na kazi kubwa kujaribu kusafisha muundo wa chama tawala unaodaiwa kujaa rushwa. Mihula miwili ya Rais Jacob Zuma yamekumbwa na madai takriban 783 ya rushwa yaliyogeuza muonekano wa chama hicho.

Changamoto ni kubwa kwa rais wa chama cha ANC Cyril Ramaphosa

Kando na hilo la kupambana na rushwa changamoto nyengine kubwa inayomkabili Ramaphosa katika uongozi wake kama rais wa chama tawala cha ANC ni kuamua iwapo rais wan chi Jacob Zuma atakubaliwa kuendelea kuiongoza nchi hadi pale uchaguzi utakapofanyika mwaka wa 2019 au iwapo atatakiwa kuachia ngazi kama ilivyofanyika kwa rais wa Zamani Thabo Mbeki.

Hata hivyo wengi wanasema  huenda wakaafikiana kuwa Zuma aachie ngazi kwa heshima ili aweze kupata msamaha ili aisweze kushitakiwa.

Rais wa chama tawala cha ANC Cyril RamaphosaPicha: Getty Images/AFP/G. Khan

Kwengineko kuchaguliwa kwa Ramaphosa kumeleta matumaini katika eneo la Soweto alikokulia ambako watu wa eneo hilo wamekatishwa tamaa na chama cha ANC. Charlie Khoza mwanafunzi wa masuala ya uandishi mwenye umri wa miaka 21 anasema Ramaphosa ni kioo cha Jamii ni mtu aliyekulia katika mji huo wa Soweto lakini akainukia kuwa mtu mmoja muhimu sana duniani.

Kwa upande wake Niseman Baleyi, mwenye umri wa miaka 39, baba wa watoto wawili na kinyonzi kwa miaka ishirikini anasema anaamini rais huyo mpya wa chama tawala cha ANC anaweza kuufufua zaidi uchumi wa Afrika kusini ambapo zaidi ya robo ya watu wake hawana ajira.

Hali ngumu ya kisiasa inayowakuta vijana wengi weusi nchini Afrika kusini inalisukuma wimbi kubwa la vijana wapiga kura mikononi mwa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) chake Julius Malema kilichowashawishi wengi kuwa utaifishaji wa madini na kugawanywa kwa ardhi kutawaondoa katika umasikini.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW