Ramaphosa mwenyekiti tena chama tawala ANC
19 Desemba 2022Hatimaye Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa chama cha African National Congress (ANC) kinachoongoza nchi hiyo tangu mwaka 1994 na hivyo kupata tena fursa ya kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2024.
Licha ya kampeni kali za kumpinga Ramaphosa, sasa wafuasi kutoka majimbo ambayo hayakumuunga mkono wanasema baada ya mgombea wao kuangushwa, watashirikiana na mwenyekiti aliyechaguliwa.
Rais Cyril Ramaphosa ameshinda kwa muhula wa pili kama kiongozi wa ANC, kwa kupata kura 2476, akimshinda Zweli Mkhize aliyepata kura 1897.
Paul Mashatile ndiye naibu rais mpyawa chama ameshinda kwa kura 2178 kutoka kwa wajumbe wanaohudhuria mkutano mkuu wa 55 wa chama hicho unaoendelea hapa Johannesburg.
Soma pia:Chama cha ANC chagawanyika katika makundi yanayomuunga mkono na yanayompinga Ramaphosa
Wakizungumza muda mfupi mara baada ya kutangazwa kwa viongozi saba wa juu wa chama hicho, baadhi ya wajumbe wa ANC waliohudhuria na kushiriki uchaguzi huo wamesema, wajumbe wamemchagua Ramaphosa ili aweze kumaliza kazi aliyoianza.
Kwa upande wake rais na mwenyekiti Mstaafu wa ANC Thabo Mbeki, mbali na kudai kuwa hajaegemea upande wowote amesema amefurahia matokeo ya uchaguzi:
Mpambano kwenye sanduku la kura
Rais Cyril Ramaphosa amemshindampinzani wake na waziri wa afya wa zamani, Dk. Zweli Mkhize, kwa tafauti ya kura 579 na anaingia awamu nyengine ya uongozi wa chama huku kikiwa kimegawanyika na kupoteza umaarufu miongoni mwa raia wa Afrika Kusini.
Hata hivyo wajumbe kutoka majimbo ambayo hayakumuunga mkono Ramaphosa, wamesema watashirikiana naye ili kuimarisha na kukijenga chama hicho kilichopambana kuiletea uhuru Afrika kusini
Baadhi ya wachambuzi katika taifa hilo ambalo mara nyingi limekuwa likishuhudia chuki dhidi ya wageni na minyukano mikali ya hoja kwa wanasiasa wanasema walitarajia juu ya matokeo hayo.
Soma pia:Wajumbe wa ANC kumchagua kiongozi
Peter Bigenda ni mchambuzi wa siasa anansema matawi mengi ya chama chake yalikuwa tayari yamekwisha mpendekeza Ramaphosa kuendelea kukiongoza chama hicho.
Chama tawala ANC kwa mara nyingine kitaongozwa na Rais Ramaphosa na makamu wake Paul Mashatile kwa miaka mingine mitano na kazi kubwa iliyopo mbele yake ni kukiunganisha na kuhakikisha kinarudisha ushawishi wake ulioanza kupungua miongoni mwa wapiga kura.
Ushindi huu tiketi ya Ikulu?
Ushindi huo unamsafishia njia Ramaphosa kuwania muhula wa pili wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, kwa sababu kwa mujibu wa katika ya Afrika Kusini rais huchaguliwa na bunge.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho tawala wapatao 4,300 wamempitisha Ramaphosa kwa kura 2,476 dhidi ya 1,897 zilizomwendea mpinzani wake, waziri wa zamani wa Afya Zweli Mkhize.
Soma pia:Kamati kuu ya ANC kuamua hatma ya Ramaphosa Afrika Kusini
Wachambuzi wanasema agenda ya Rais Cyril Ramaphosa kufanya mageuzi makubwa ndani ya ANC zitakumbana na upinzani mkali kutoka kwa maafisa wapya waliochaguliwa katika uongozi wa chama hicho.